Baada ya Jukwaa la Fursa za Biashara na Maonesho ya Teknolojia ya Dhahabu kurindima Mkoani Geita, wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje ya Geita wameendelea kujitokeza kuwekeza kwakuwa mkoa unayo mazingira rafiki ya uwekezaji kwani kwetu urasimu ni mwiko.
Tarehe 14.11.2018, Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amefungua kiwanda kidogo cha kuzalisha chaki cha ELIMU BORA STANDARD CHAKI GEITA kinachomilikiwa na kampuni ya Lugwisha Company Ltd ambayo pia inajihusisha na uuzaji wa mbao pamoja na utoaji huduma ya hoteli iliyopo maeneo ya Shilabela, kilichopo Mtaa wa Mine Mpya, Kata ya Bombambili Halmashauri ya Mji Geita huku akiwa na furaha kwani azma ya mkoa ni kuvutia wawekezaji na kwamba Geita muda si mrefu itakua na kituo kikubwa cha biashara hivyo mwitikio huu ni dalili njema Geita.
Amesema, “kwanza nampongeza mkurugenzi wa kiwanda hiki na kwa kuunga juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Rais Dkt. Magufuli, na ametengeneza historia kwakuwa ndicho kiwanda cha kwanza tangu mkoa wa Geita uzaliwe na zina viwango hazina vumbi ambapo awali tulizipata mbali lakini sasa zipo hapa”. Lakini pia kama serikali na wataalam wa biashara ni jukumu letu kumsaidia mwekezaji bidhaa hizi zifike nje ya nchi” ahaidi kumsaidia mwekezaji kutafuta soko kisha akaandika ubaoni neno “hapa kazi tu” kama ishara ya kuzindua chaki hizo
Bado Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi wote wakaribie kuwekeza Geita, maeneo yapo na Geita haina urasimu wala rushwa bali mwekezaji hupokelewa na kupatiwa huduma kwa kadri ya hitaji lake.
Ameendelea kusema kuwa anaamini atazikuta chaki hizo kwenye maduka yote yanayouza bidhaa za elimu akikumbusha kuwa uzalendo ni pamoja na kutumia vya nyumbani huku akitoa wito kwa wamiliki wa taasisi za elimu zilizoshiriki hafla hiyo kuunga mkono juhudi za muwekezaji huyo kwa manufaa ya Geita
Akisoma taarifa ya mradi kwaniaba ya uongozi wa kiwanda hicho, Bw. Msuka Charles alisema dhumuni kubwa la mradi huo ni kuwaleta watanzania wa Mkoa wa Geita pamoja hususani wadau wa sekta ya Elimu kujivunia bidhaa zitokazo ndani ya Mkoa na kuingiza kipato chenye manufaa ya Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Bw. Msuka ameongeza kusema,“mradi huu wenye dhamira ya kukuza uchumi na kuongeza ajira katika Sekta binafsi, ulianzishwa tarehe 10/10/ 2017 kwa kufanya upembuzi yakinifu na wakina kuhusu mradi huu na kuomba kibali cha ujenzi tarehe 20/10/2017 kisha kufanikiwa kupata kibali cha ujenzi tarehe 17/11/2017 na ujenzi kuanza tarehe 21/11/2017 kwa garama inayokadiriwa kuwa Shilingi 106,000,000/= (milioni mia moja na sita za kitanzania) na ujenzi bado unaendelea lakini pia tumeanza kazi ya uzalishaji wa chaki tarehe 1/8/2018”
Pia bw. Msuka ameeleza uwezo wa uzalishaji wa kiwanda hicho akisema, “kiwanda hiki kimeandaliwa kwa uzalishaji wa chaki. Mashine hufanya kazi masaa 16 kwa siku na huweza kuzalisha chaki 448,000 ambazo ni sawa na boksi 4,480 zenye vipisi 100 kila boksi, hivyo kwa siku tunazalisha katoni 149 zenye boksi 30 kila katoni moja. Kwa mwezi tunazalisha katoni 4,470 na kuweza kuendelea kukidhi mahitaji ya Mkoa na Mikoa jirani.
Kwa upande wake Mhe. Leonard Bugomola, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita na Diwani wa Kata hiyo ya Bombambili amemshukuru mwekezaji huyo mzalendo ambaye aliona kiwanda hicho akiweke Geita lakini pia kuweza kutoa ajira kwa wana Geita. Pia ameahidi kuwa Halmashauri anayoiongoza itakuwa mteja wa kwanza kuunga mkono juhudi za mwekezaji huyo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya Ndg. Barnabas Mapande kwa upande wake amempongeza mwekezaji huku akisema “tunahitaji Tanzania ya viwanda na viwanda vyenyewe ndio kama hiki, hongera sana na tutakuunga mkono”
Kaimu Mkurugenzi wa Mji Geita Bw. Adolph Ritte akatumia fursa hiyo kutangaza uwepo wa maeneo mengi ya uwekezaji hivyo wananchi na wawekezaji wanazidi kukaribishwa Geita.
Mkurugenzi na mmiliki wa Kiwanda hicho Bw.Sylvester Lugwisha amemshukuru mkuu wa mkoa kwa kukubali kufungua kiwanda chake huku akimuahidi kuwa kampuni yake ipo tayari kushirikiana na uongozi wote kuanzia ngazi ya mtaa na kwamba watalipa kodi zote zinazostahili huku wakiboresha maslahi ya wafanyakazi.
Miongoni mwa walioshiriki hafla hiyo ni kamati ya Fedha na Mipango ya Madiwani, wataalam kutoka sekretarieti ya mkoa na halmashauri bila kusahau wananchi
Awali, Mhe.Mhandisi Gabriel alipokea taarifa, kisha kukata utepe na kutembelea eneo la uzalishaji kujionea shughuli hiyo inavyofanywa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa