KATIBU TAWALA MKOA WA GEITA AZINDUA HUDUMA ZA MADAKTARI BINGWA MKOANI GEITA
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita ndugu Selestine Gesimba amezindua huduma za madaktari bingwa mkoani Geita na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kupata huduma hizi muhimu kwa maendeleo ya afya zao.
Akizungumza katika uzinduzi huo ambao umefanyika katika hospitali Teule ya Mkoa wa Geita Gesimba ametoa rai kwa watumishi wa Hospitali hiyo ambao watapata fursa ya kushirikiana na madaktari bingwa kujifunza mbinu mpya ili baadae wawasaidie wananchi wenye matatizo mbalimbali ya afya. ’’Uwepo wa madaktari bingwa awa katika hospitali yetu ya mkoa ni fursa nzuri sana kwa wataalamu wetu kujifunza mbinu mpya za utoaji wa huduma za matibabu pasipo kwenda kujifunza mbinu hizo nje ya maeneo ya kazi. Hivyo, natoa rai kwa wataalam wetu wote watakaoshirikiana moja kwa moja na mabingwa awa katika utoaji wa huduma, kutumia nafasi hiyo kujifunza kutoka kwao ili hata watakapoondoka mbakie na ujuzi wa kuwahudumia wananchi wetu’’.
Aidha, amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kwa kujitokeza kwa wingi na kufanyiwa uchunguzi ili wapate huduma bora kwa kuwa huduma hizi zinapatikana mbali na maeneo yao kwa gharama kubwa. Pia amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa kuhakikisha anafanya tathimini ya vifaa katika Hospitali na vituo vya afya vyote ili kuona namna ya kupata mkopo wa vifaa tiba kutoka Mfuko wa taifa wa bima ya afya na kuboresha huduma katika Hospitali na vituo hivyo.
Awali akimkaribisha Katibu Tawala Bi. Aifena Mramba Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF ambaye pia ni Mkurugenzi wa tiba wa NHIF amesema kuwa Mfuko huo umeona umehimu wa kupeleka huduma za madaktari bingwa karibu na wananchi ili wapate huduma hizo kwenye maeneo yao pasipo kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo. Aidha Mfuko huo umetoa mashuka 100 kwa ajili ya wodi za hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita. Jumla ya madaktari bingwa 8 wa aina tofauti za magonjwa wanatoa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa