Wataalam wa Kampuni ya China CAMC Engineering iliyopata zabuni kujenga kituo cha kupoozea umeme Geita eneo la mpomvu, tayari wamewasili mkoani Geita tayari kwa kuanza ujenzi wa mradi huo baada ya zoezi la fidia lililokuwa likiendelea kukaribia tamati.
Akiongea kwa niaba ya wataalam alioambatana nao katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Bw. Lane Lei amesema yeye na wenzake wamefurahi kufika Geita na wameyapenda mazingira huku akihaidi kuifanya kazi hiyo kwa muda uliopangwa ili kutatua kero ya wana Geita iliyokuwapo kwa muda mrefu sasa ya kukatika kwa umeme .
Amesema, “ tumefurahia kuwa Geita ni wakarimu na ni mahala salama, tumependa mchele wa huku ni mzuri na nafuu na tunakushukuru mkuu wa mkoa kwa kutupokea. Tutapenda na tupo tayari kufanya kazi ya jamii mkoani hapa kwani popote tunapofanya kazi ni lazima tuache kitu. Vilevile tutakuwa tayari kufanya kazi na wazawa wa Geita na Watanzania kwa kazi zilizopo kulingana na uhitaji”. alimaliza
Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel akachukua fursa hiyo kuwahakikishia ulinzi na ushirikiano muda wote wawapo Geita lakini pia awaomba wasisite kujulisha kwa eneo lolote watakalokwama ili aweze kuwasaidia lengo ni kutekeleza mradi kwa wakati akiwaambia “nitafuteni masaa 24 nitakua tayari kuwasaidia”
Awali Waziri wa Nishati Mhe. Dkt.Medard Kalemani alimleta na kumtambulisha Mkandarasi huyo CAMC Engineering of China Mkoani Geita na kumuonesha eneo hilo tarehe 17.07.2018 ambapo lilifuata zoezi la fidia ili kuanza kwa ujenzi wa mradi huo na kwa kuwa ni mzoefu, Waziri Kalemani alisema anaamini atafanikisha utekelezaji wake tena kwa wakati, ufanisi na kasi inayozingatia ubora. Mhe. Waziri anaamini mradi huo utakamilika ifikapo Mei, 2019 kwa maana Mhe. Rais Magufuli tayari amewezesha mradi huo kwa kutoa Dola Milioni 123 za Kimarekani (123,000,000.USD) sawa na zaidi ya Shilingi Bilioni Arobaini za Kitanzania.
Tukumbuke kuwa, serikali katika kutafuta suluhisho la kudumu la tatizo la umeme ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM, inajenga Kituo kikubwa cha Kupozea umeme (Sub Station) ambacho kitaanza kujengwa wiki ijayo eneo la Mpomvu Mjini Geita, eneo lenye ukubwa wa takribani heka tano kitakachokuwa na uwezo wa 220/33KV, 2x50MVA ambazo ni takribani Megawati 96 yaani kitapokea Umeme wa Msongo wa Kilovolt 220 na kutoa Kilovolt 33 kisha kuvinufaisha vijiji kumi na moja (11) vitakavyopitiwa na mradi, na wakazi 1,424 walio jirani. Mikoa jirani kama Mwanza na Kagera itaweza kunufaika umeme huu kwani ni wa kutosha.
Kati ya Megawati 96, Mgodi Mkubwa wa Dhahabu GGM utapewa Megawati 20, na zitakazobakia ni kwa wananchi. Kwa maana nyingine, wawekezaji endeleeni kuukaribia mkoa huu kwa kuwa mazingira rafiki ya kufanya biashara yanapatikana lakini Mgodi waa GGM waarifiwa kuendelea kujiandaa kupokea Megawati hizo kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli zao na kwa kufanya hivyo watakuwa wanafanya kazi kwa tija na kuchangia pato la taifa kwa kutumia umeme wa TANESCO.
Hiyvo basi, Serikali ya Mkoa inaendele kutoa shukrani za dhati kwa Mhe. Rais na Wizara ya Nishati kwa ujumla kwa kuhakikisha ahadi hii inatekelezwa, lakini pia wito unatolewa kwa wananchi kuitunza miundombinu hiyo wakati na baada ya kukamilika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa