HALMASHAURI MKOANI GEITA ZATAKIWA KUJENGA MAGHALA
Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoani Geita zimetakiwa kuweka utaratibu wa kujenga maghala ambayo yatamilikiwa na Mamlaka hizo ili wananchi watunze mazao na kuongeza mapato kwa ajili ya utoaji wa huduma za maendeleo.
Akizungumza katika kikao cha kujadili hoja za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ambacho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa, Mhe. Ezekiel Kyunga Mkuu wa Mkoa wa Geita amezitaka Mamlaka hizo kujenga maghala ili wananchi watunze mazao katika maghala yaliyojengwa na Halmashauri ambayo yatatokana na kodi zao wenyewe. Mkuu wa Mkoa amesema kuwa njia hii itasaidia kupunguza gharama za kuhifadhi mazao katika maghala binafsi, pia itakuwa rahisi kukabiliana viashilio vya uhaba wa chakula.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amewataka Wakuu wa Wilaya kusimamia na kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuhifadhi chakula walichokipata kwa kuacha tabia ya kuuza chakula hovyo. Vilevile ametumia kikao hicho kuzitaka Halmashauri kuimarisha minada na kuhakikisha kuwa watu wote wenye mifugo katika hifadhi wanaondoka katika hifadhi hizo wao pamoja na mifugo na kurudi walikotoka.
Katika kikao hicho Katibu Tawala wa Mkoa ndugu Selestine Gesimba amewataka watumishi wa Umma Mkoani humu kufuata sheria, taratibu na kutoa ushirikiano kwa wakaguzi wa hesabu za Serikali pale wanapotekeleza majukumu yao na amewasii kuwa wazalendo kwa taifa na kuacha tabia zinazokinzana na kanuni za Utumishi wa Umma.
Na: Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa