Mgodi wa Dhahabu Geita utapunguza gharama zake za uendeshaji kwa asilimia 92% baada ya kuanza kutumia umeme wa gridi ya Taifa kupitia kituo chake cha kupokea na kupoza umeme cha msongo wa kilovoti 33/11.
Mgodi wa GGM ambao ulianza kufanya kazi mwaka 2000 umekuwa ukitumia nishati ya umeme wa mafuta ambao umekuwa ukipelekea gharama za uzalishaji kuwa juu Zaidi na kuzalisha kwa kasi hewa ya ukaa ambayo ni hatari kwa mazingira.
Akizindua rasmi Kituo cha Kupokea na kupoza umeme cha Geita Gold Mine tarehe 13/8/2024, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilifanya uamuzi wa kushirikiana na GGM katika ujenzi wa Kituo hicho ili kuupunguzia mzigo Mgodi wa Dhahabu Geita kama mchangiaji mkubwa wa mapato ya Serikali ambaye amekuwa akitumia gharama kubwa ya uendeshaji kwa sababu ya kutumia mafuta.
Mhe.Dkt. Biteko ameupongeza Mgodi wa GGM kwa kuingiza gridi ya Taifa katika mgodi wao kwa ushirikiano walioutoa katika kuhakikisha ujenzi wa kituo hicho unakamilika na Serikali kugharamia ujenzi wa laini yenye urefu wa kilomita sita kutoka Kituo cha Kupoza Umeme Cha Mpomvu. Pia ametoa wito kwa Wizara ya Nishati na Taasisi zote za Serikali kuendeleza ushirikiano na Sekta binafsi ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi na kuchangia mapato ya Serikali.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujenga mazingira rafiki kwa wa wawekezaji ikiwemo kutoa fedha Zaidi ya shilingi Bilioni 8 ili kuwezesha ujenzi wa line ya umeme kutoka eneo la Mpomvu hadi Mgodi wa GGM pamoja na kupeleka umeme katika maeneo mengine ya wachimbaji wadogo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini Mhandisi Abubakar Issa ameeleza kuwa kuanza kazi kwa kituo hicho kutaipatia GGM umeme wa uhakika na kuongeza ufanisi katika shughuli za uchimbaji na uzalishaji wa Dhahabu pamoja na kuongeza mapato ya TANESCO kwa kuwauzia GGM umeme wa Megawati 34.
Kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Geita Gold Mine kimejengwa kwa gharama ya Dola 25.8 milioni sawa na shilingi za kitanzania Bilioni 67.08 ambapo Mgodi wa GGM umejenga kituo na Serikali kutoa fedha za usogezaji wa line ya umeme ya kilomita sita.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa