Katika kuimarisha vyama vya ushirika nchini kupitia mikoa, mkuu wa mkoa wa Geita Mhe.Rosemary Senyamule amekabidhi pikipiki tatu zilizotolewa na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa maafisa ushirika kama vitendea kazi ili kuimarisha sekta hiyo.
Makabidhiano hayo yamefanyika Juni 24, 2022 katika eneo la EPZA Bombambili halmashauri ya mji Geita na kuhudhuriwa na wananchi pamoja na maafisa ushirika ambapo mkuu wa mkoa ameelekeza utunzwaji wa vyombo hivyo vya usafiri ambavyo ni vitendea kazi lakini pia kuimarisha ushirika kwenye halmashauri za mkoa wa Geita.
“tumshukuru na kumpongeza sana Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa haja ya kupatikana vitendea kazi. Kazi ya pikipiki hizi ni kwa ajili ya kuimarisha ushirika hivyobasi sitegemei kuona migogoro mingi ya ushirika ofisini kwangu” amesema Mhe.Senyamule
Vilevile, mkuu wa mkoa amesema ni matumaini yake kuwa pikipiki hizo zitatumika kwa kazi kusudiwa akikemea vyombo hivyo kutumiwa na mtu akiwa amelewa na kwamba viendeshwe kwa umakini mkubwa akiagizwa viegeshwe kwenye maeneo salama.
Akitoa maelezo ya awali, Bi Doreen Mwanri ambaye ni Mrajis Mkoa wa Geita amesema, “hizi ni juhudi za Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kupitia wizara ya kilimo, chakula na ushirika kwa kutoa pikipiki hizi kwenye sekta ya ushirika, tunamshukuru sana. Hivyo, moja ya sharti la pikipiki hizi ni kufanya shughuli za vyama vya ushirika na zimetolewa kwa ajili ya halmashauri za wilaya za Mbogwe, Nyang’hwale na Geita”
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya Geita Mhe.Barnabas Mapande amesema “tunamshukuru mhe.Rais kwa juhudi za kuwahudumia wananchi kwakuwa katika kipindi chake kwani amefanya mambo mengi katika kipindi kifupi hivyo tumuombe MUNGU aendelee kumlinda na kumbariki”
Aidha, mkuu wa wilaya ya Geita Mhe.Wilson Shimo ameendelea kuishukuru serikali kwa kuendelea kuwajali wananchi kwani kupitia pikipiki hizo wananchi watafikiwa na hivyo kupunguza changamoto.
Akishukuru kwaniaba ya maafisa ushirika, Bw.Jonis Rweyunga ambaye ni afisa ushirika mwandamizi kutoka Nyang’hwale amesema anaishukuru serikali inayoongozwa na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kuwajali na kutambua mahitaji yao na wanaahidi kuzitumia vizuri kama ilivyokusudiwa na kuzitunza kwakuwa umuhimu wa ushirika ni wa juu sana kwenye maendeleo ya wananchi
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa