Leo Desemba 10, 2021 Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Rosemary Senyamule amefanya ziara kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'hwale kukagua Utekelezaji wa Ujenzi wa Miradi ya Ujenzi wa Madarasa kwa fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya Uviko 19.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amewapongeza viongozi wa Halmashauri hiyo kwa usimamizi mzuri wa miradi ya Ujenzi wa Madarasa kwani kwa wastani shule zote wametekeleza kwa zaidi ya 83% na kwamba hadi kufikia Desemba 15, 2021 wana mikakati kukamilisha hadi kuweka Samani kwenye madarasa.
"Tuna kitu cha kujifunza kutoka kwenye Shule hii maana kwenye maeneo mengine sijaona Miundombinu ya walemavu kuingilia kwenye madarasa lakini hapa nimeona leo, na nawasihi wengine waliodhani wataweka mwishoni wasije wakasahau jambo hili muhimu," amesema Mhe. Mkuu wa Mkoa akikagua ujenzi kwenye shule ya Sekondari Izunya.
Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa ameonesha furaha yake kwa Utekelezaji mzuri wa miradi ya Ujenzi wa Vituo vya Afya kutoka Fedha za Tozo kwani Halmashauri hiyo imetekeleza kwa kasi na viwango bora na amezitaka Halmashauri zingine kuiga mfano huo na kuhakikisha ifikapo Desemba 31, 2021 wakamilishe vituo hivyo.
"Kingine cha kuwapongeza Nyang'hwale ni ujenzi wa miradi ya Vituo vya Afya kutoka kwenye Fedha za Tozo, pamoja na ujenzi wa Madarasa nyie mmeonesha kuwa Miradi ya Serikali inaenda kwa pamoja hivyo na Halmashauri zingine ambao wamekua wazito naomba wajifunze hapa," amesema.
"Idara ya Elimu Sekondari ilipokea jumla ya Tshs. Milioni 800 kwa ajili ya Ujenzi wa vyumba vya madarasa 40 na Tshs. Milioni 280 kwa ajili ya vyumba vya madarasa 14 katika shule za Msingi Nne Shikizi." Amesema Mkuu wa Wilaya ya Nyang'hwale, Mhe. Jamhuri Wiliam.
Aidha, Mhe. Mkuu wa Wilaya amebainisha changamoto ya samani na milango kupatikama kwa shida kidogo lakini amesema wanatarajia kuzitatua na kwenda na wakati."Changamoto tuliyonayo Mhe. Mkuu wa Mkoa ni madawati na kasi ya utengenezaji wa milango tumeona siyo nzuri sana ila tunaendelea kufuatilia kwa karibu ili tuweze kukamilisha kwa wakati."
"Mhe. Mkuu wa Mkoa, shule hii ilipokea Tshs. Milioni 60 kwa ajili ya Ujenzi wa vyumba vya Madarsasa 3, Mradi huu utapunguza Utoro kwa wanafunzi na utaongeza wataalamu nchini kwa faida ya Taifa letu" Mwalimu Deogratiana Mwangalaba, Mkuu wa Shule Izunya Sekondari.
Mhe. Mkuu wa Mkoa shule ya Sekondari Msalala tulipokea Tshs. Milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa Vyumba 4 vya madarasa lakini tunatekeleza Ujenzi wa vyumba 4 vya Madarasa na Ofisi Moja kwa ubora unaokusudiwa kwa Tahs. Milioni 80 hiyohiyo na tutabakisha na kiasi kidogo cha Fedha." Mpuya Mlyakado, Mkuu wa Shule ya Msalala.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa