Na. Boaz Mazigo - Geita
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan inaendelea kudhihidirisha jinsi inavyowajali wananchi wake katika kuhakikisha inalinda afya zao.
Hayo yamethibitishwa mkoani Geita Aprili 27, 2023 wakati wa utambulisho wa mfumo wa m-mama, mfumo maalum kwa ajili ya rufaa na usafiri wa dharura kwa wajawazito, waliojifungua na watoto wachanga.
Akifungua mkutano wa kuutambulisha mfumo huo, mkuu wa mkoa Geita Mhe.Martine Shigela amesema “ ninaishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kupitia OR-TAMISEMI, Wizara ya Afya na wadau wa maendeleo kwa kufanikisha na kuikisha m-mama mkoani Geita. Huu ni wakati muafaka kwa mkoa wetu kuwa na mfumo huu unakuja kutatua changamoto ya vifo vitonavyo na uzazi”
Mhe.Shigela aliongeza kuwa, “ uzazi ni furaha na heshima na siyo ugonjwa, hivyo kama serikali mkoani Geita , tutahakikisha tunawalinda mama wajawazito ili kupunguza vifo".
Sambamba na hilo, Mhe.Shigela alisisitiza juu ya mkoa kuhakikisha inazingatia suala la lishe huku akiwapongeza wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Geita kwa kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya masuala ya lishe akisema ni vyema kuendelea kujitathmini na kuweka mikakati ili kuhakikisha mkoa unaendelea kusonga mbele kwenye masuala ya lishe.
Katibu tawala mkoa Geita Prof.Godius Kahyarara alisisitiza kuwa, Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe.Rais.Dkt.Samia imewekeza sana kwenye afya, ni vyema wananchi kuipongeza na kama mkoa “tutafanya kazi kwa pamoja kuufanikisha mfumo wa m-mama”
Kwa upande wao Dkt.Charles Kato ambaye ni mratibu mfumo wa m-mama kanda ya ziwa wa Shirika la Pathfinder International, Bi.Linda Deng ambaye ni Mkurugenzi wa Mradi-Touch Foundation na Bi.Rahma Bajun ambaye ni mkuu wa m-mama Tanzania kwaniaba ya mdhamini (VODACOM) kwa nyakati tofauti, wote walionesha furaha na shukranio kwa mapokezi waliyoyapata Geita na kuahidi kupata matokeo na kwamba watafanya kazi na serikali kwa ushirikiano.
Kwaniaba ya halmashauri za wilaya mkoani Geita, mwenyekiti wa halmashauri ya Mji Geita Mhe.Charles Kazungu alisema, wanaishukuru serikali kwa kuleta m-mama, wanaikaribisha na maelekezo yote yatatekelezwa na kwamba wataendelea kutenga bajeti kwenye masuala ya lishe na wanaamini mfumo huo utaleta suluhu ya changamoto za vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga.
Mfumo wa m-mama ni mfumo utakaomwezesha mwananchi kupata usafiri wa kumfikisha mgonjwa katika kituo cha kutolea huduma kwa dharura
m-mama, Karibu Mkoani Geita tuokoe uhai wa wajawazito, waliojifungua na watoto wachanga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa