Na Boazi Mazigo - Geita
Mkuu wa mkoa geita Mhe.Martine Shigela ametoa rai kwa waajiri wote mkoani geita kuzingatia suala la mafunzo kwa wafanyakazi ikiwa ni sehemu ya kuboresha maslahi na mazingira bora kwa mfanyakazi ili kuongeza tija na ufanisi kwenye taasisi, shirika au kampuni.
Rai hiyo imetolewa Mei Mosi, 2023 wakati akizungumza na wafanyakazi kutoka taasisi za umma na binafsi mkoani Geita baada ya kupokea maandamano yao wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani Mei Mosi ambapo kwa mkoa wa geita imeadhimishwa katika uwanja wa CCM Kalangalala na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.
RC Shigela alisema, serikali inayoongozwa na Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan inawajali wafanyakazi na ndiyo maana imeendelea kuboresha maslahi yao na kwamba, ili taasisi ziweze kukabiliana na changamoto mpya za kimaendeleo katika utendaji, ni vyema waajiri kuzingatia kuwapa mafunzo wafanyakazi wake kama sehemu ya kuongeza ufanisi na kuwataka waajiri ambao hawajaanza kutekeleza maelekezo ya serikali ya kima cha chini cha mshahara kufanya hivyo mara moja.
“viongozi, ni vyema muwajengee uwezo wafanyakazi walio chini yenu, kuna mabadiliko duniani, hivyo ni muhimu kuwa na bajeti zinazojumuisha watenda kazi kupata mafunzo wawapo kazini. Mbali na hilo, niwaombe waajiri kujenga mazingira mazuri kwa wafanyakazi kwani ni vizuri kumfanya huyu mfanyakazi ajihisi ni sehemu ya taasisi kwa jinsi unavyomtendea na kumjali” alisema RC Shigela.’
Pamoja na kusema hayo, RC Shigela alihimiza juu ya haki na wajibu kwa pande mbili kati ya muajiri na muajiriwa akimaanisha kuwa, wafanyakazi nao wana wajibu wa kufanya kazi kwa weledi na ubunifu ili kuongeza ufanisi katika taasisi na kwamba kwa hali hiyo, kama kila mmoja akifanya sehemu yake basi maslahi nayo yataendelea kuboreshwa. Pia alisisitiza juu ya wafanyakazi kutofanyishwa kazi sizizo na staha, kuzingatia utu na taratibu katika kuwajibishana pale inapotokea changamoto kwa mfanyakazi kama ambavyo katiba ya nchi inavyothamini utu, na mwisho akagawa vyeti vya watumishi hodari pamoja na zawadi kwa washindi wa michezo mbalimbali.
Awali akizungumza kwaniaba ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi TUCTA Geita, katibu wa TAMICO Bw.Obed Mwakapango alisema bado ziko changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi ikiwemo malimbikizo, taasisi binafsi kutozingatia viwango vipya vya mishahara, baadhi ya waajiri kutopeleka michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii n.k na kuiomba serikali kuingilia kati suala hilo ili kuendelea kuboresha maslahi ya mtumishi
Naye katibu tawala mkoa Geita Prof.Godius Kahyarara alisema, “ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan, mengi yamefanyika kwa watumishi hivyo hatuna budi kumshukuru. Kama mkoa tunasisitiza juu ya ajira zenye staha, lakini tuhakikishe tunawajibika ipasavyo na kutimiza wajibu ili iendane na kudai maslahi”. Alimaliza kisha kuwapongeza wafanyakazi walioshiriki siku hiyo adhimu.
Kwaniaba ya CCM Mkoa Geita, Bi Mary Mazula aliwapongeza watumishi wote akiwasifu kwa utendaji kazi na kutoa wito kwa sekta binafsi kuhakikisha zinazingatia maelekezo ya kima cha chini cha mshahara na kwamba kama chama tawala ni wasikivu na wataendelea kupambania haki na stahiki za wafanyakazi.
“Hakika Mishahara Bora na Ajira za Staha ni Nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi, na Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan, Amethibitisha”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa