Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe.Rosemay Senyamule amezindua uhifadhi na utunzaji Mto Nikonga ikiwa ni jitihada za serikali kupitia bodi ya maji ya bonde la ziwa Tanganyika chini ya wizara ya maji kuhifadhi vyanzo vya maji nchini.
Uzinduzi na uhifadhi huo umefanyika Juni 25, 2022 katika kata na kijiji cha kamena ulipo Mto Nikonga ndani ya halmashauri na wilaya ya Geita, mto ambao ni miongoni mwa kidakio cha mto Malagarasi, huku mkuu wa mkoa huyo akisisitiza juu ya wananchi kutekeleza sheria ya uhifadhi vyanzo vya maji, kutunza vyanzo vya maji na kwamba ni muhimu wananchi kutambua kuwa maji ni rasilimali adimu waitunze.
Akiongea wakati wa uzinduzi huo RC Senyamule alisema “maji ni rasilimali isiyo na mbadala, tutunze vyanzo vyetu kwa pamoja. Tuwe pamoja na si mmoja mmoja kwenye hili. Kumekuwa na upungufu wa maji kwakuwa vyanzo vingi vinaharibiwa, hivyo tushikamane kuhifadhi chanzo hiki” .
Aliongeza kwa kuiagiza Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) mkoa wa Geita kuhakikisha wanapanda miti rafiki wa maji kwa kushirikiana na uongozi wa kamena na baadaye kuwakumbusha wananchi wa kamena kuhakikisha hawafanyi shughuli za kibinadamu ndani ya mita sitini (60) kama ilivyoelezwa kwenye sheria kisha kutembelea chanzo na kuzindua uhifadhi kwa kusimika bango na nguzo.
RC Senyamule alimaliza kwa kuwakumbusha wananchi kujiandaa kuhesabiwa pale zoezi la sensa ya watu na makazi litakapoanza ifikapo agosti 23, 2022 pamoja na kujiandaa kushiriki kwenye mbio za mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu ambapo kwa mkoa wa Geita zinatarajiwa kuanza Julai 20, 2022
Awali akisoma taarifa ya mradi, mwakilishi wa mkurugenzi wa bonde la ziwa Tanganyika mhandisi Odemba Cornel alisema, Mto Nikonga ni mojawapo ya kidakio kidogo cha mto Maragarasi na kwamba mto huo ni miongoni mwa mito inayokabiliwa na uchafuzi wa mazingira na maji kwa kiasi kikubwa kutokana na shughuli za kibinadamu zinazofanywa ndani ya mita 60 ambazo ni hifadhi ya mto kwa mujibu wa sheria ya mazingira fungu la 57 na sheria ya rasilimali za maji namba11 ya mwaka 2009 kifungu cha 34 na kwamba mradi huo ulitengewa kiasi cha Milioni 420 ili kuhifadhi na kuutunza mto huu na matawi yake kuanzia kijiji cha Kamena hadi pori la Bukombe/Ushirombo ambao una urefu wa takribani km 55.
Mhandisi Odemba aliongeza kuwa, miongoni mwa faida za mto Nikonga ni pamoja na kuwa ni mto pekee unaotegemewa na wakaazi zaidi ya 70,000 waishio kandokando ya mto huo kwa mujibu wa taarifa ya kijiji na ni mto unaotengeneza ikolojia inayopendeza hasa katika maeneo ya hifadhi kama misitu ya Rwamgasa, Ushirombo na Kigosi na kwamba mto huu huchangia kiasi kingi cha maji katika mto Moyowosi, Malagarasi na Ziwa Tanganyika.
Aidha, mhandisi Odemba alihitimisha kuwa “pamoja na umuhimu wa mito hii kwa jamii yetu, bado inakabiliwa na changamoto kama matumizi holela kwa shughuli za uchenjuaji madini, kilimo na ufugaji, uzuiaji wa mto (ili kuvua samaki) hali ambayo huondoa uwiano wa matumizi ya maji baina ya watumiaji, upungufu wa maji, maji kujaa matope n.k”.
Nao Mhe.Alhaj Said Kalidushi ambaye ni mwekiti wa CCM mkoa wa Geita, Mhe.Wilson Shimo, DC Geita na Mhe.Peter Ndekela, diwani wa Kamena kwa nyakati tofauti waliwasihi wananchi kutekeleza shughuli hiyo na kwamba baada ya uzinduzi huo kamati ya usalama wilaya itakuwa ikipita kuhakikisha hakuna shughuli mpya inaanzishwa kama kilimo kwenye eneo la hifadhi ili kuendelea kutunza chanzo hicho.
Bonde limepanga kutekeleza uhifadhi na utunzaji kwa kuweka alama kuanzia Kamena hadi Kashishi urefu wa Km 10, ambapo nguzo 400 na mabango 20 vitasimikwa pande zote za mto na pia bonde limeanzisha jumuiya ya mto Nikonga ukanda wa juu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa