Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Ndugu Mohamed Gombati amepokea taarifa ya utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) ambayo imewafikia wananchi 161,154 katika Mkoa wa Geita.
Katibu Tawala Mkoa wa Geita ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya dhati ya kuleta kampeni hii kwa wananchi kwa lengo la kuwasaidia kupata huduma mbalimbali za kisheria ambazo zimekuwa zikiwatatiza kwa kipindi kirefu pasipo kupatiwa ufumbuzi kwa sababu ya uwezo mdogo wa kifedha kwa wananchi walio wengi kulipia gharama za Mawakili.
“ Kampeni hii imekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Geita kwa sababu imeweza kutatua migogoro ya ardhi na mipaka iliyodumu kwa miaka mingi pamoja na migogoro mingine ya kijamii. Napenda kumshukuru Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na wataalam wake kwa kuwaongezea ujuzi wa kazi za utatuzi wa migogoro mbalimbali Maafisa wa madawati waliopo mkoani kwetu.” Aliongeza Ndg. Mohamed Gombati.
Ndg. Mohamed Gombati ametumia wasaa huo kutoa mwaliko kwa Wizara ya Katiba na Sheria kutumia fursa ya Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika Mkoani Geita kila mwaka kwa kushiriki na kuendelea kutoa elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria kwa wananchi.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Mratibu wa Kampeni kwa Mkoa wa Geita Wakili wa Serikali Bw. Candid Nasua amesema hadi kufikia Februari 4, 2025 walifanikiwa kukamilisha zoezi la Kampeni ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia ambapo wamefika katika Halmashauri zote sita,Kata, Vijiji na Mitaa iliyopangwa na kuwezesha migogoro 86 kutatuliwa papo kwa papo na migogoro 498 inaendelea kushughulikiwa ili kuipatia ufumbuzi.
Kampeni ya Mama Samia Legal Aid iliyofanyika kwa siku tisa iliambatana na utolewaji wa huduma ya usajili wa matukio muhimu ya binadamu iliyotolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini( RITA) ambapo jumla ya wananchi 721 wamefikiwa na huduma hiyo. Pia kulifanyika zoezi la uchangiaji damu salama, upimaji wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele, uchunguzi wa Saratani ya mlango wa kizazi na huduma ya uzazi wa mpango.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa