Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameongozana na mamia ya waombolezaji katika kuusitiri mwili wa marehemu dada yake Bibi. Monica Joseph Magufuli (miaka 63) nyumbani kwake kijiji cha Mlimani Wilayani Chato Mkoani Geita tarehe 21.08.2018.
Kipekee, Mhe. Dkt. Magufuli amewashukuru viongozi na wananchi mbalimbali waliojitokeza kushiriki katika ibada ya mazishi ya dada yake mpendwa bila kumsahau shemeji yake na mme wa marehemu ndugu. Stanslaus Madulu kwa kukubali kumruhusu marehemu Monica kukaa na mama yake mzazi kabla ya umauti kumfika, kisha kuwaongoza kuaga mwili wa marehemu pamoja na mazishi ya dada yake.
Amesema, “ na hili leo nataka niwaambie kitu cha pekee alichokuwa nacho Monica; pamoja na kutambua kuwa alikuwa na mume wake, watoto tisa na wajukuu ishirini na tano, aliamua kuja kukaa na mama. Akamuomba mume wake na mume wake akaridhia; nami kwa heshima kubwa namshukuru sana shemeji yangu kwa kumruhusu dada yetu kuwa anakuja kukaa na mama kitu ambacho kwa wanaume wa kisasa ni kigumu”. Hivyo Monica amekuwa wa pekee sana kwa maisha ya familia na kifo chake kimeniachia maswali ambayo siwezi kuyajibu kwa urahisi kwa mama.”alimaliza.
Baada ya mazishi, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Rais Ikulu ndugu. Gerson Msigwa kwa niaba ya familia ya Mhe. Dkt. Magufuli alisoma wasifu wa marehemu, kisha kutoa shukrani kwa wote walioweza kushiriki tukio hilo.
Miongoni mwa walioshiriki ibada hiyo ya mazishi ni pamoja na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kasim Majaliwa Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Wahe. Marais Wastaafu, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Raila Amolo Odinga, Mwakilishi wa Rais wa Burundi, Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wahe. Mawaziri, Wahe. Wakuu wa Mikoa, Wahe. Wabunge, Wahe. Wakuu wa Wilaya, Maaskofu, Mabalozi, Viongozi wa Chama Tawala CCM, Katibu Tawala wa Mkoa, Wahe. Wenyeviti wa Halmashauri, wakurugenzi, Wakuu wa Idara na wananchi.
Marehemu ameacha mgane, watoto tisa, na wajukuu ishirini na tano. Bwana Ametoa na Bwana Ametwaa, Jina Lake Lihimidiwe.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa