Jumla ya viongozi wa wizara nane (8) wamewasili Mkoani Geita kwa lengo la kuangalia na kutatua changamoto za ardhi ikiwemo migogoro mbalimbali, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt, John Pombe Magufuli kusitisha mara moja zoezi la kuviondoa Vijiji na Vitongoji vinavyodaiwa kuwepo katika maeneo ya hifadhi na kuzitaka Wizara zote zinazohusika kukutana ili kubainisha na kuanza mchakato wa kurasmisha maeneo ya Vijiji na Vitongoji hivyo.
Baada ya kupata taarifa ya utangulizi iliyoonesha uhitaji wa jumla ya Hekta za eneo elfu thelathini na mbili (32,000) pamoja na kilometa thelathini (km30) kutoka eneo la mpaka wa hifadhi kuingia ndani ya hifadhi, kiongozi wa msafara huo wa wahe. Mawaziri, Mhe. William Lukuvi (Mb) ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongozana na Mwenyeji Mkuu wa Mkoa wa Geita kuongea na wananchi wa Bwanga,Wilayani Chato kuwaeleza lengo la ziara hiyo, waliokusanyika kwa wingi baada ya ugeni huo kuwasili katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Magufuli tarehe 18.02.2019.
Waziri Lukuvi amewaeleza wananchi kuwa, ”geita ni miongoni mwa mikoa iliyoathirika sana na hifadhi ya misitu kwakua asilimia sabini na tano (75%) ya ardhi ya mkoa huu iko kwenye hifadhi za misitu. Tunatambua mna ardhi kidogo, hivyo kwa maagizo ya Mhe. Rais Magufuli ya kuwapa wananchi ardhi inayowatosheleza kufanya shughuli za kilimo na ufugaji, tutafikisha maombi yenu yaliyowasilishwa na viongozi wenu ambayo tunaamini yatajibiwa na tunawapongeze kwa kuwa ninyi Chato mliheshimu na vijiji kumi na sita (16) vimepisha msitu, viko nje vimebanana sana”.
Mhe. Lukuvi akachukua fursa hiyo kuwaomba wananchi kuwa wavumilivu wakati wakisubiri majibu ya maombi yao ya ardhi yatakayofikishwa kwa Mhe. Rais Magufuli akiwaomba wasivamie misitu ili kusubiri kupangwa upya watakaporejea tena ili kila kijiji kiwe na eneo lake linalotambulika na wakulima na wafugaji waweze kufanya shughuli zao bila shida yoyote, huku akiwataka viongozi kusimamia wakati huu wa mpito kisha viongozi hao wakaendelea na safari.
Awali, mwenyeji wa ugeni huo Mhe. Mhandisi Robert Gabriel aliwaongoza wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama kuupokea ugeni na kisha kufanya kikao kidogo ukumbini na kutoa taarif fupi kabla ya viongozi hao kuwasalimia wananchi.
Nao Wakuu wa Wilaya za Chato na Bukombe mahali penye changamoto hizo za ardhi wakapata fursa ya kueleza maeneo wananchi wanayohitaji kupewa, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhe. Eng. Mtemi Msafiri aliainisha uhitaji wa eneo la ukubwa wa Hekta 19,000 kutokana na uwepo wa vijiji 16 pembezoni mwa hifadhi ya msitu wa Biharamuro- Kahama na Kwa upande wa Bukombe, Mkuu wa Wilaya Mhe. Said Nkumba akaainisha uhitaji wa eneo la Hekta 13,000 pamoja na km.30 kutoka mpaka wa hifadhi hiyo kuingia ndani.
Ugeni huo Mkoani Geita ulijumuisha Waheshimiwa Mawaziri nane (8), yaani Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Waziri Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Naibu Waziri Kilimo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira na Waziri Maliasili na Utalii.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa