Na Boazi Mazigo, Geita RS
Mkuu wa mkoa Geita Mhe.Martine Shigela amekabidhi na kuzindua gari la wagonjwa (ambulance) na kuelekeza Halmashauri kuhakikisha gari hiyo linafanya kazi iliyokusudiwa hususan kuokoa maisha ya wananchi, inatunzwa na kutengenezwa kwa wakati ili kutimiza adhma ya serikali ya kuwahudumia wananchi.
Amekabidhi gari hiyo Novemba 23, 2023 wakati wa ziara yake ya kikazi katika kituo cha afya masumbwe kilichopo Halmashauri ya wilaya mbogwe huku akiwakumbusha watumishi wa afya kuendelea kuwahudumia wananchi kwa lugha za staha na kwamba serikali inawathamini sana.
"tunamshukuru rais wetu mhe.dkt.Samia Suluhu Hassan na jinsi anavyotuonesha upendo kwa kuiboresha sekta ya afya kupitia miundombinu, vifaa tiba pamoja na watumishi na leo tunakabidhi na kuzindua gari la wagonjwa. Gari hii itunzwe na ifanye lengo kusudiwa kuwahudumia wananchi, hivyo faraja ya kiongozi aliyetoa gari hii yenye vifaa vya kisasa ni kuona linatunzwa", alisema RC Shigela.
RC Shigela alimaliza kwa kukata utepe ishara ya kuzindua gari hiyo na kuupongeza uongozi wa wilaya akiamini kuwa itatunzwa.
Kwa upande wake mganga mkuu mkoa Dkt.Omari Sukari alisema, gari hiyo ni kati ya gari sita zitakazoletwa Geita ambapo kwa awamu ya kwanza mkoa huu uliletewa gari mbili kwa ajili ya wilaya ya Nyang'hwale na Mbogwe na kwamba serikali pia imetoa gari 5 kwa ajili ya ufuatiliaji shughuli za afya, hivyo kuendelea kuipongeza serikali kwa kuwajali wananchi kwakuwa jambo hilo husaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.
Mwisho, Mkuu wa wilaya hiyo Mhe.Sakina Mohamed alimshukuru Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan kufuatia fedha na uwekezaji mwingi unaofanyika mbogwe kuanzia miundombinu, watumishi na vifaa kisha kuahidi kutunza vifaa vyote ikiwemo gari hiyo na kwamba itafanya kazi iliyokusudiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa