Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Geita wameridhishwa na kuipongeza halmashauri ya wilaya ya Mbogwe kufuatia utekelezaji mzuri wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ile itokanayo na fedha za Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19
Hayo yamejili leo desemba 13, 2022 wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Geita wilayani Mbogwe ambapo wajumbe hao wameonesha kuridhika na jinsi halmashauri hiyo ilivyojitahidi kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali kumi (10) ikiwemo ya elimu, afya, maji na barabara ambayo yote kwa pamoja imehidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni mbili, milioni mia tano sitini sita, laki sita thelathini na tisa na mia nne ishirini na tano (2,566,639,425) huku wakihimiza mshikamano na usimamizi thabiti kwa miradi mingine inayoendelea kutekelezwa ndani ya halmashauri hiyo ambapo hadi sasa miradi hiyo kumi (10) iliyotembelewa imekwisha kutumia jumla ya shilingi bilioni moja, milioni arobaini na tano, laki saba sitini na moja na mia nane na moja (1,045, 761,801) huku wakisisitiza wananchi kuwahimiza watoto kuhudhuria shule.
Akizungumza katika ziara hiyo, ndg. Evarist Gervas, kiongozi wa msafara, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapindizi (CCM) Taifa kutoka mkoa wa Geita amesema kuwa, Mbogwe imejitahidi kufanya kazi kwa viwango huku akisisitiza kujiandaa na ujenzi wa shule maalum ya sekondari ya mfano itakayojengwa katika kata ya Bunigonzi.
“Mbogwe niwapongeze sana, mmejenga na kusimamia vizuri sana. Niombe ushirikiano na usimamizi mliouonesha kwenye usimamizi wa miradi hii, muuoneshe hata wakati wa ujenzi wa shule maalum ya sekondari itakayojengwa Bunigonzi ambayo itajengwa kwa shilingi milioni mia nne sabini (470,000,000) zilizotolewa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakika tunamshukuru sana” alisema MNEC Evarist.
Katika hatua nyingine, katibu wa CCM Mkoa Bibi.Alexandrina Katabi aliwasihi wananchi kuwahimiza wanafunzi kuhudhuria shuleni lakini pia upandaji wa miti utakaoisaidia shule kuwa na mazingira mazuri na hewa safi huku pia akimshukuru Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya chama tawala yaani CCM.
Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Mhe.Mhandisi Charles Kabeho ambaye katika ziara hiyo amemwakilisha pia mkuu wa mkoa wa Geita amesema kuwa, serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi katika kuhakikisha inasimamia yale yote yaliyoelekezwa kwenye ilani ya CCM ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia viwango, weledi na thamani ya fedha ili kuleta matokeo chanya.
Naye bw.Shihumbi Mateyo ambaye ni Mwananchi wa kata ya Bukandwe ameishukuru serikali inayoongozwa na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaletea wananchi fedha nyingi za maendeleo, huku akisisitiza kukamilishwa kwa nyumba ya mtumishi katika zahanati hiyo ili iweze kufanya kazi na kuwahudumia.
Miradi hii kwa ujumla wake itasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kuwafanya waaalimu kufundisha kwa njia shirikishi kwa uwepo wa kundi dogo ndani ya darasa kwa upande wa shule. Vilevile kwa upande wa afya, itapunguza changamoto nyingi za kiafya kwa kusogeza huduma ya afya karibu, kupunguza vifo vya akina mama wajawazito lakini pia kuvutia huduma nyingine za kijamii. Bila kuacha sekta za maji na barabara ambazo kwa kiasi kikubwa zitachochea uchumi kutokana na watu kuwa na afya bora wanapotumia maji safi na salama lakini pia kutokupoteza muda mwingi wakitafuta maji, huku uwepo wa barabara nzuri ukirahisisha ufanyaji wa biashara, usafirishaji na usambazaji bidhaa, ambavyo hakika ni faida lukuki zapatikana.
Vilevile ziara hiyo ilihusisha wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya, wataalam kutoka ofisi ya mkurugenzi Mbogwe, watalaam kutoka ofisi ya katibu tawala mkoa wa Geita pamoja na wananchi wa maeneo husika ilipokuwa miradi.
Ziara hiyo itaendelea kwenye halmashauri za Mji na Wilaya Geita.
GEITA YA DHAHABU, UTAJIRI NA HESHIMA
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa