Serikali katika Mkoa wa Geita imeeleza kuwa Mfumo wa Usafirishaji wa Dharura kwa akina mama wajawazito, waliojifungua ndani ya siku 42 na watoto wachanga wenye umri hadi siku 28 (m-mama) utaendelea kutoa huduma na kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa ili lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi liweze kufikiwa.
Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Geita Ndg. Herman Matemu alipokuwa mgeni rasmi wakati wa kikao cha makabidhiano ya mfumo wa m-mama kutoka kwa wadau pamoja na kujadili mpango kazi wa uendelevu wake kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita hivi karibuni.
Ndg. Herman Matemu ametoa shukrani za dhati kwa Serikali ya awamu ya sita na wadau wote wa maendeleo ambao ni Vodacom, Touch Foundation na Pathfinder International kwa kuimarisha mfumo wa m-mama na kuwezesha jumla ya kina mama 3511 na watoto wachanga 538 kusafirishwa tangu ulipoanza utekelezaji katika mkoa wa Geita mwezi Juni 2023.
Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Geita amesema kuwa ili mfumo huu uendelee kusimama imara na kufanya kazi Halmashauri zote za Mkoa wa Geita zinatakiwa kuhakikisha Bajeti za usafiri wa dharura kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga pamoja na gharama za ufuatiliaji zinajumuishwa katika bajeti kuu za Halmashauri kwa kila mwaka.
Mwakilishi wa Shirika la Pathfinder International Bw. Uriel Kinuma ametoa shukrani kwa namna Serikali ilivyoshirikiana nao kama wadau katika kuhakikisha wanapunguza vifo vya wajawazito, waliojifungua na watoto wachanga kwa kuimarisha mfumo wa rufaa na usafiri wa dharura kwa gharama nafuu na kwa kutumia teknolojia tangu ulipoanza kazi katika Mkoa wa Geita na ana matumaini kuwa wadau wanapoukabidhi rasmi kwa Serikali utaendelea kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Kwa upande wa mratibu wa m-mama Mkoa wa Geita Bi. Jasintha Boniphace amesema tangu mfumo ulipoanza kazi katika mkoa huo wamefanikiwa kutoa elimu kuanzia ngazi za vijiji hadi Mkoa ikijumuisha Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali kubwa, Kupata madereva ngazi ya jamii ambao wameshaingia mikataba na wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na kuwasafirisha wagonjwa Zaidi ya 4049.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa