Katika kuimarisha na kurahisiha upatikanaji wa bidhaa za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini na kupunguza hoja za kiukaguzi katika ununuzi wa bidhaa za afya kwa kupitia utelekelezaji wa Sera ya Public Private Partinership (PPP), Ofisi ya Rais – TAMISEMI ilitoa waraka na. 1 wa mwaka 2018 ambao ulielekeza matumizi ya Washitiri Teule wa Mikoa katika ununuzi wa bidhaa za afya pale vituo vinapokosa bidhaa hizo MSD kupitia mfumo wa Prime Vendor Management Information System (PVMIS).
Utekelezaji waraka huo umeifanya timu ya wataalam kutoka OR-TAMISEMI kuendesha mafunzo ya siku tatu kwa wataalam mbalimbali mkoani Geita kuanzia Machi 14 hadi16, 2023 katika ukumbi wa mikutano ofisi ya mkuu wa mkoa (Magogo) kwa lengo la kupata wawezeshaji wa Mkoa na Halmashauri (T.O.Ts) wa Mfumo wa Mshitiri, ambao hao watafundisha matumizi ya mfumo huo ngazi za vituo vya afya.
Akifungua mafunzo hayo kwaniaba ya mkuu wa mkoa Geita, Bw.Herman Matemu ambaye ni kaimu katibu tawala mkoa amesema upatikanaji wa dawa na vipimo vya kitabibu kwa uhakika katika kituo cha huduma, kwa kiasi kikubwa unaakisi ubora wa huduma zinazotolewa na mahali hapo, hivyo amemshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuipongeza Serikali anayoiongoza kwa kuendelea kutoa fedha nyingi katika kuimarisha utoaji wa huduma za Afya ngazi ya Msingi nchini.
Bw. Matemu ameongeza kuwa kwa kutambua hilo, Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali ili kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya unakuwa asilimia 100% ikiwemo Mfumo wa Mshitiri na uwepo wa mfumo huo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi CCM 2020, kama ilivyoainishwa katika sura ya tatu, sehemu ya 81 (i) na (aa) hivyo kuwataka watumiaji kukusanya mapato kuweza kwaulipa Washitiri kwa wakati mara baada ya kupokea shehena ya bidhaa, kuepushe madeni yasiyo ya lazima.
"nina Imani kutokana na mafunzo haya, sote tutaondoka na uelewa wa pamoja wa utekelezaji wa mwongozo wa mfumo wa huu ili tuweze kuusimamia kikamilifu kwa ajili ya kuleta matokeo sahihi. Tukasimamie ukusanyaji wa mapato katika vituo vya kutolea huduma za Afya, ili viweze kulipa Washitiri kwa wakati mara baada ya kupokea shehena ya bidhaa, kuepushe madeni yasiyo ya lazima”. Alimaliza bw.Matemu
Mwisho, aliwaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia kikamilifu afua mbalimbali za Mfumo wa Ugavi wa bidhaa za afya ikiwemo kufanya Medicine Audit mara kwa mara katika vituo vya kutolea huduma, kwa ajili ya kupunguza changamoto zinazotokana na usimamizi mbovu wa bidhaa hizo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, bw.Amiri Mhando ambaye ni mjumbe wa kitaifa wa kamati ya uratibu ya Prime Vendor System (PVS) amesema katika mafunzo hayo, washiriki watajifunza utekelezaji wa Mfumo wa Mshitiri (Prime Vendor System) kwa kupitia Mwongozo wa Utekelezaji wa Mfumo wa Mshitiri (Prime Vendor System Implementation Manual) pamoja na mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa taarifa za Mshitiri (Prime Vendor Management Information System) ili kuweza kuwafundisha na kuwasimamia watoa huduma juu ya utekelezaji wa mfumo huu.
Naye mganga mkuu mkoa dkt.Omari Sukari amesema kwa kushirikiana na wataalam hao, watahakikisha lengo la serikali linatimia na hatimaye kuimarisha upatinaji wa bidhaa za afya.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na wakurugenzi wa halmashauri, maafisa ugavi na ununuzi, maafisa TEHAMA, wafamasia na waganga wakuu kutoka halmashauri zote za mkoa wa geita
.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa