Na Boazi Mazigo. Geita RS
Wananchi mkoani Geita wametakiwa kuendeleza tuna zilizoasisiwa na viongozi wa Taifa la Tanzania zilizoasisiwa na Hayati Baba wa Taifa Mwl.Julius Kambarage Nyerere na kwamba kupitia amani, umoja na mshikamano kunakuwa na umoja wa kitaifa.
Rai hiyo imetolewa Desemba 9, 2023 na Mkuu wa Mkoa Geita Mhe.Martine Shigela wakati akiendesha kongamano la kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara lililofanyika katika kimkoa katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi kwa makundi mbalimbali wakiwemo wazee, vijana, viongozi wa chama na Serikali.
Akiongea kabla na baada ya kongamano hilo, RC Shigela ameupongeza uongozi wa wilaya hiyo kwa maandalizi ya maadhimisho hayo huku akishukuru misingi iliyowekwa na chama cha TANU ambayo imeendelezwa na Chama Cha Mapinduzi CCM ya binadamu wote ni sawa kuthamini utu wa mtu, kuheshimiana n.k
"Nchi yetu ni ya kujivunia sana na kila mmoja hujisikia huru ni kutokana uwepo wa misingi ya Kidemokrasia.Taifa letu limekua kimbilio la uwekezaji ni kwa sababu kuna mazingira rafiki na amani na ndiyo maana hatubaguani hata kwa itiikadi za vyama", Alisema RC Shigela.
Akiwa kama mgeni rasmi, RC Shigela alihitimisha kwa kuwakumbusha wanachi akisema, " tunaye Rais wetu Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, mwenye upendo wa dhati na taifa la Tanzania, anasimamia fedha na tunaziona zinaletwa mikoani. Zamani kwenye bajeti tulitegemea kwa asilimia takribani 80 lakin leo tumekusanya kama nchi mapato ya kujiendesha kwa zaidi ya asilimia 60, tumpongeze"
Akitoa salam za Chama Cha Mapinduzi, Katibu wa CCM Mkoa wa Geita Bi.Alexandrina Katabi alisema, wanamshukuru Mungu kwa kuiona miaka 62 ya Uhuru na CCM itahakikisha kwa NAMNA NA HALI yoyote inailinda Amani ya Nchi hii kwakuwa bila Amani hakuna Maendeleo, hakuna uwekezaji, umoja, na hakuna mshikamano banana ya Watanzania, hivyo ni muhimu kuilinda Amani iliyopo nchini.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Said Nkumba alisema, anawashukuru wote waliochangia mada wakiwemo wanafunzi na kuahidi kuwa serikali inaendelea kuboresha maisha pamoja na elimu na kwamba kwa mwaka 2024/25 wanatarajia kujenga bweni la shule kama yalivyokuwa maombi ya wanafunzi wengi.
DC Nkumba ameeleza pia upo mpango kuhakikisha Shule zote za Sekondari na vituo vya kutolea huduma za afya ambazo hazina umeme vitapata umeme wa jua (solar).
Kila ifikapo Desemba 9 ya tangu mwaka 1961, Tanzania Bara (awali ikiitwa Tanganyika) imekua ikiadhimisha siku ya uhuru wake kwa aina tofauti tofauti.
Kwa mwaka 2023, Tanzania imeadhimisha sherehe hizo kitaifa Jijini Dodoma na kuzindua Mchakato wa Ukusanyaji Maoni Kutoka kwa Wananchi Kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, lakini pia kila mkoa ulitakiwa uadhimishe kwa kufanya kongamano kama ambavyo mkoa wa Geita umefanya katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe kwa kuendesha kongamano
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa