Ndoto ya Mhe. Lolesia Bukwimba, Mbunge wa Jimbo la Busanda, ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita ya kuwa na shule ya sekondari ya ghorofa imeonekana kuanza kutimia baada ya harambee iliyofanyika katika kijiji cha Nyalwanzaja, Kata ya Nyalwanzaja, Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuwezesha kupatikana kwa Milioni 34, mgeni rasmi akiwa mkuu wa mkoa wa geita mhandisi Robert Gabriel Julai 2, 2019.
Akiwapongeza wananchi na wadau mbalimbali wakiwemo Mgodi wa Dhahabu Geita (GGML) waliounga mkono wazo la mbunge Bukwimba baada ya kuzindua uchimbaji msingi wa ghorofa hilo, baada ya kuendesha harambee, Mhandisi Gabriel amesema, hawezi kukaa kimya kuelezea juhudi zinazofanywa na mbunge wao katika kuwaletea maendeleo na kuwapongeza viongozi wa ngazi zote wa Chama Tawala na Serikali akiwaasa kushikamana kuendelea kutekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo.
“nipo geita kwa miezi ishirini, nimejifunza mengi na sipaswi kukaa kimya, nawapongeza uongozi wa wilaya ya geita. Msikatishwe tamaa na wasio wema na wanaowabeza kwa maana hata ukiwa unaogelea, wapo watakaosema unawatimulia vumbi. Mbunge wenu anafanya kazi kama tembo, hana makelele lakini kazi ni kubwa inayoonekana. Ninaamini ghorofa hili kupitia wananchi kuleta mchanga, mawe, na mafundi pamoja na maji litakamilika kwa miezi minne na si sita kama ambavyo mmepanga”asema mhandisi Gabriel.
Amemaliza kwa kushukuru uongozi madhubuti wa CCM kupitia viongozi wa mkoa na wilaya alioambatana nao, ambao amekuwa akikutana nao kila alipoenda kuchimba misingi ya miundombinu ya elimu na afya akisema anashuhudia utekelezwaji wa Ilani kwa vitendo.
Kaimu Katibu wa CCM Mkoa Odilia Batimayo amesema, chama kinatambua jitihada zinazofanywa na mbunge Bukwimba pamoja mhandisi Gabriel pamoja na usimamizi kwenye halmashauri ikiwa ni utekelezaji wa vitendo wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015, jambo linalowapelekea kama chama kuahidi kutoa mchango wa hali na mali ikiwemo saruji pamoja na nguvu kazi ya vijana itakayoratibiwa chini ya katibu wa UVCCM wilaya ya Geita Ally Rajabu, huku katibu wa CCM Wilaya Mohamed Ally akizidi kushuhudia ushirikiano baina ya viongozi wa chama na serikali ikiwa yeye ni mgeni ndani ya mkoa huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ali Kidwaka ameeleza shukrani zake kwa wizara kutoa kibali cha ujenzi wa ghorofa hilo na kuhanganua michango itakayowezesha ujenzi akisema, “serikali kuu Milioni 40, halmashauri imetenga Milioni 40 kwenye fedha za CSR zinazotokana na mgodi wa GGM, hivyo kufanya jumla kuu pamoja na mchango wa harambee kufikia milioni 114”. Amesema atahakikisha ujenzi unasimamiwa vyema kwa kuzingatia thamani na kwamba jamii itambue kuwa halmashauri hiyo ina uhitaji mkubwa hivyo kazi kubwa imefanyika.
Ujenzi huu utakuwa wa vyumba vitatu juu na chini kwa majengo matatu (3blocks) japo kwa sasa umeanza ujenzi wa awamu ya kwanza kwa kujenga jingo moja la vyumba 6, vitatu juu vitatu chini. Pia serikali kuu imewezesha mil 50 kwaajili ya nyumba ya watumishi.
Ni maono ya mkoa na mbunge Bukwimba kuwa, shule hiyo itawasaidia wanafunzi hasa wa kike kuepuka vishawishi kwakuwa itawapunguzia umbali lakini pia ujenzi huo ni mwanzo wa ndoto ya mkoa kujenga hosteli nyingi iwezekanavyo.
Pamoja na mchango wa Mbunge Bukwimba na Mkuu wa Mkoa Mhandisi Gabriel, wadau mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita Leonard Bumogola, wahe. Madiwani, Wachimbaji wa wadogo kutoka Nyarugusu, wananchi, wakuu wa idara, wafanya biashara na viongozi mbalimbali wa Chama Tawala na wa Serikali wamejitoa kufanikisha harambee hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa