Zaidi ya wananchi laki sita waishio katika maeneo ya vijijini ndani ya Mkoa wa Geita wamenufaika na ujenzi wa minara 55 ya mawasiliano iliyojengwa na inayoendelea kujengwa katika Wilaya za Nyang’hwale, Geita, Bukombe, Mbogwe na Chato Mkoani humo.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa ziara ya ukaguzi wa minara hiyo, Mkurugenzi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) Bi. Justina Mashiba ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa ruzuku ya shilingi Bilioni 6.44 kwa ajili ya ujenzi wa minara ya mawasiliano kwa teknolojia ya 2G, 3G na 4G ambapo mpaka sasa watanzania 643,354 katika Mkoa wa Geita wamenufaika.
Bi. Mashiba ameongeza kuwa kupitia mfuko wa UCSAF Serikali imeingia makubaliano na watoa huduma za mawasiliano kujenga minara 2,185 Nchi nzima ambapo Zaidi ya wananchi milioni 23 wanaoishi katika vijiji 5,111 watanufaika na mradi huu mara utakapokamilika.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuupatia Mkoa wa Geita fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa minara ya mawasiliano ambayo itaboresha hali ya mawasiliano kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya vijijini.
Mhe. Shigela ameeleza baadhi ya faida zitakazopatikana kupitia uboreshwaji wa mawasiliano vijijini ni pamoja na kufungua fursa za biashara kwa wananchi waishio katika maeneo hayo ambao wanafanya shughuli mbalimbali za kiuchumi kama kilimo, ufugaji, uvuvi ambao baada ya kupata mawasiliano yenye uhakika wataweza kujitangaza kibiashara kupitia simu janja za mkononi na kupata wateja pasipo kutumia nguvu kubwa.
“Ndugu wananchi wenzangu wa mkoa wa Geita ambao mmeshapata minara katika maeneo yenu, ninawasihi kuitunza vizuri ili baadhi ya vijana wetu wapate ajira ndogo ndogo kupitia minara hiyo pia wakulima, wavuvi, wafugaji na wananchi wengine mtapata fursa ya kuongeza uchumi na kujipatia maendeleo binafsi na jamii nzima kupitia simu zenu za mkononi.” Aliongeza Mhe. Shigela.
Mfuko wa Mawasiliano kwa wote ulianzishwa kwa lengo la kufikisha huduma za mawasiliano vijijini na mjini kusiko na mvuto wa kibiashara. Mkoa wa Geita ni moja kati ya mikoa ambayo ni mnufaika wa mradi ambapo ujenzi wa minara 55 unaendelea katika Wilaya ya Bukombe minara 10, Chato minara 9, Halmashauri ya Wilaya ya Geita minara 10, Mbogwe minara 18 na Nyang’hwale minara 8. Mpaka kufikia mwezi Julai 2024 Minara sita kati ya 55 inayojengwa imeshawashwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa