Hakika, huu ni ukurasa mpya kwa Mkoa wa Geita ambapo ni siku ya ishirini na nne sasa tangu apatikane Mshindi wa Mashindano ya Ulimbwende yani Miss Geita na kuamua kumtembelea Mkuu wa Mkoa wa Geita tarehe 14.08.2018 akiwa ameambatana na wenzake wawili kwa ajili ya kupangiwa kazi za kufanya kuitumikia jamii ya Geita lakini pia kujitambulisha.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amefarijika kuona namna Mlimbwende huyo na mwakilishi wa Mkoa wa Geita katika kipengele cha urembo akiwa na wenzake walivyotambua umuhimu wa kazi na kuona urembo si mavazi pekee bali hata kufanya kazi za jamii.
Amewaeleza warembo hao kuwa, “kwenye urembo, suala muhimu ni kujitambua, na urembo ni kioo cha jamii; hivyo mnapaswa kujua kuwa jamii inawategemea”.
Pia Mhe. Mhandisi Gabriel amefurahishwa na namna walimbwende hao walivyo na mikakati ya kuendelea na masomo kwani wote ni wasomi jambo linalouthibitishia umma kuwa, urembo si watu wa sitaki shule.
Mkuu wa Mkoa akatumia fursa hiyo kuwakaribisha kufanya kazi za Mkoa na kumuelekeza Afisa Michezo kuweka ratiba ya kuzitembelea shule za Mkoa wakianzia shule za bweni kwa awamu tofauti ili kutoa elimu kwa wanafunzi juu ya kuepuka mimba wangali wanasoma.
“nimefurahishwa na kauli yenu ya urembo mwaka huu inayosema “Urembo na Kazi Kwa Maendeleo ya Jamii” kwa kuwa inaenda sambamba na kaulimbiu ya Mhe. Rais ya Hapa Kazi Tu,
hivyo ninaahidi ushirikiano kwenu na nitaambatana nanyi kwenda kutoa elimu nikiwa kama mgeni rasmi mtakaponialika kwenye shule zetu”, alimaliza.
Naye Bi. Joyce Magesa ambaye ni Miss Geita mwaka 2018 kwa niaba ya wenzake Bi Angel David ambaye ni Mshindi wa pili bila kumsahau Bi. Natalie David Mshindi wa Tatu, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ukubali wake kushirikiana nao na kusema pamoja na kazi za jamii watakazozifanya, wanao mpango wa kuanzisha taasisi ya misaada (foundation) ambayo si ya kiserikali yani (NGO) itakayowasaidia watoto waishio mazingira magumu na wanaofanyishwa kazi wangali wadogo, hivyo kuomba ushirikiano watakapokuwa tayari kuanzisha taasisi hiyo.
Afisa Habari kutoka Wizara Mlezi ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi Anitha Jonas amefurahishwa na uamuzi wa warembo hao na kusema yeye kama miongoni mwa walezi anawaasa kuzingatia maadili na kulinda heshima kwani jamii nayo inajufunza mengi kutoka kwao. Pia amewaeleza msimamo wa serikali wa kuzingatia weledi kwani ni taa ya kuwaongoza kufikia mafanikio
Afisa Michezo wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa ndugu Caroli Steven akasema, kwa upande wake kuwa, anaahidi kushirikiana nao na kusema atapanga ziara ya kuzitembelea shule za sekondari za Mkoa wa Geita ili kutoa elimu kwa pamoja kama alivyoelekezwa na Mkuu wa Mkoa.
Hakika Mkoa unajivunia kuwapata walimbwende wenye mtazamo kama huu, hawa ni mfano wa kuigwa na walimbwende wengine Tanzania.
Karibuni Jukwaa la Fursa za Biashara linaloanza tarehe 15.08.2018 na kuisha tarehe 16.08.2018.
Karibuni Jukwaa la Fursa za Biashara linaloanza tarehe 15.08.2018 na kuisha tarehe 16.08.2018.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa