Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila amemuagiza Mkandarasi Sichuan and Bridge Cooperation Limited kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa kilomita 17 za Barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wa Geita ndani ya muda uliopangwa.
Mhandisi Mativila ametoa agizo hilo hivi karibuni alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa Kilomita 17 za Barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wa Geita ambao unatekelezwa kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Miji Tanzania( TACTIC) chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.
Naibu Katibu Mkuu ameeleza kuwa baada ya ukaguzi wa mradi huo amebaini kuwa ujenzi wa Barabara pamoja na ofisi ya mkandarasi uko nyuma ya muda kutokana na nguvu kazi hafifu, ukosefu wa vitendea kazi na kupelekea mradi huo ambao unapaswa kukamilika Februari 2025 kuonyesha ishara za kutofikia malengo ya kukamilika kwa muda na kuwanyima wananchi fursa ya kupata huduma ya barabara.
“ Mradi uko nyuma kwa asilimia 26, ulitakiwa uwe umefikia asilimia 60 kwa sasa ukijumuisha jengo pamoja na barabara, lakini mpaka sasa umefikia asilimia 34 pekee kinyume na makubaliano ya kimkataba. Kwa mantiki hiyo, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Sichuan ambaye yuko Nchini China anatakiwa kuja Tanzania ndani ya muda wa wiki mbili ili kutoa maelezo ya kina namna watakavyopambana kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya muda uliopangwa kabla ya Serikali kuchukua hatua nyingine dhidi yao.” Aliongeza Mhandisi Mativila.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Mtaa wa Uwanja Kata ya Nyankumbu, Ndg. Japhet Jorado amesema kuwa ujenzi wa Barabara ya Nyankumbu- Kivukoni umekuwa ukisuasua sana na kusababisha usumbufu kwa waendesha vyombo vya moto ambao wametengenezewa njia mchepuko nyembamba na yenye kona kali iliyodumu kwa kipindi kirefu kutokana na ujenzi wa daraja unaoendelea.
Ndg. Japhet Jorado ameeleza pia hofu yake ya kuanza kwa kipindi cha mvua huku barabara zikiwa hazijakamilika kutasababisha wananchi kukosa kabisa huduma ya barabara kwa sababu ya ubovu mkubwa wa barabara inayopita katika mtaa wao ambayo kwa sasa imekwanguliwa lakini bado haijatengenezwa.
Kwa upande wake Mhandisi Mshauri wa Mradi wa TACTIC Mjini Geita, Lucas Nyaki amesema kuwa wao kama washauri wameshaketi vikao viwili vikubwa na mkandarasi na kumuelekeza anachotakiwa kufanya ili kunusuru hali iliyopo kwa sasa lakini hawajafuata maelekezo hivyo anaishukuru Serikali kwa kuingilia kati katika utatuzi wa changamoto zinazoukabili mradi huo.
Mradi wa ujenzi wa Kilomita 17 za Barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wa Geita unatekelezwa kwa Shilingi Bilioni 22.23 ikiwa ni miongoni mwa miji 12 itakayonufaika na awamu ya kwanza ya mradi wa TACTIC Kati ya Halmashauri 45 zitakazonufaika na mradi kwa Nchi nzima.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa