Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Martine Shigela ametoa pongezi za dhati kwa wasimamizi wa Miradi ya TASAF kwa kuuwezesha Mkoa wa Geita kuwa Mkoa wa kwanza Kanda ya ziwa kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya miundombinu inayotekelezwa kwa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Nchini (TASAF).
Mhe. Shigela ametoa pongezi hizo hivi karibuni alipokuwa akizungumza katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa miradi ya TASAF ndani ya kipindi cha miaka 5, Kikao ambacho kimefanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Geita amewataka waratibu na wakurugenzi kuhakikisha miradi inakamilika kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha Juni 30 sambamba na kusisitiza umuhimu wa manunuzi kwenda sambamba na malipo ya mafundi ili kazi zilizopangwa ziweze kukamilika kwa wakati.
Akisoma taarifa ya mapokezi ya fedha za TASAF, Katibu Tawala wa Mkoa Geita Ndg. Mohamed Gombati ameeleza kuwa Mkoa wa Geita katika kipindi cha miaka 5 umepokea Zaidi ya shilingi Bilioni 58 kutoka TASAF, ambapo kati ya fedha hizo shilingi Bilioni 5.3 ni kwa ajili ya walengwa 37,688 kupitia mpango wa uhawilishaji fedha na shilingi 18 Bilioni zimetumika kutekeleza miradi ya maendeleo ya kijamii.
Katibu Tawala Mkoa Geita ameongeza kuwa Mkoa umeongezewa Shilingi Bilioni 18 baada ya kufanya vizuri kwenye utekelezaji wa miradi katika Wilaya za Chato na Mbogwe kwa ajili ya miradi ya afya na elimu ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kupunguza umaskini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba amesema kuwa TASAF imechangia kupunguza utoro katika shule ya Sekondari Izumacheli baada ya kujengewa mabweni ya wanafunzi waliokuwa wakitumia mitumbwi kuvuka maji kila siku kwenda shule na kurudi nyumbani. Pia ametoa ushauri kwa Halmashauri kutenga kwenye bajeti fedha za asilimia 10 ambayo huwa inaongezwa na jamii wakati wa utekelezaji wa miradi ya Tasaf.
Mpango wa TASAF kwa Mkoa wa Geita umewezesha wanafunzi Zaidi ya 89,000 kupata mahitaji ya shule na watoto 7,582 walio na umri chini ya miaka mitano kuhudhuria kliniki kwa ajili ya huduma na elimu ya malezi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa