Mkoa wa Geita Waagizwa Kusimamia Mabaraza ya Ardhi
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. Angelina L. Mabula ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Geita kuhakikisha Mabaraza ya Ardhi yanayoundwa katika Halmashauri zilizoko katika Mkoa yanasimamiwa vyema ili kutekeleza majukumu yaliyokusudiwa.
Agizo hilo limetolewa wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara yake kilichowajumuisha viongozi wa Mkoa wa Geita pamoja na Wataalam wa Idara ya Ardhi katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita tarehe 29/8/2017.
Mh. Angelina Mabula amesema kuwa Halmashauri za Mkoa wa Geita zinatakiwa kuwapa mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa mabaraza ya ardhi wanaochaguliwa ili watambue wajibu wao ikizingatiwa kuwa wajumbe hao hujumuisha watu mbalimbali ambao hawana elimu ya ardhi, hivyo mafunzo hayo yatawapa uelewa wa majukumu yao.
Katika kuhakikisha suala hilo linafanikiwa, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema kuwa Wizara yake iko tayari kushirikiana na Halmashauri kutoa mafunzo ya namna ya kuwapa elimu ya awali wajumbe wa Mabaraza ya ardhi ya Kata na Vijiji. Hivyo Halmashauri zisisite kuwasiliana na Wizara ya Ardhi pindi watakapohitaji huduma hiyo.
Mh. Angelina Mabula ametoa pongezi kwa Halmashauri zote za Mkoa wa Geita kwa utayari wa kushirikiana na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Ambapo Halmashauri zote zimeshatenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu. Pia ameziagiza Halmashauri zote za Mkoa wa Geita pamoja na Shirika la nyumba la Taifa kufanya ufuatiliaji wa vikundi vilivyopatiwa mafunzo ya kufyatua matofali ili kubaini mashine za vikundi ambavyo havifanyi kazi zichukuliwe na kupelekwa katika vikundi vinavyofanya kazi.
Katika ziara yake ndani ya Mkoa wa Geita Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitumia fursa hiyo kuwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote na Wataalam wa Idara ya Ardhi katika Mkoa wa Geita kuhakikisha Mfumo wa Usimamizi na Ukusanyaji kodi za Ardhi kielektroniki unatumika kikamilifu ili kuwezesha ukusanyaji wa mapato unaokidhi malengo yaliyopangwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa