Mkoa wa Geita umepokea Zaidi ya shilingi Trilioni 1.4 kutoka katika Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha kuanzia Machi 2021 hadi Juni 2025 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika sekta za afya, elimu, miundombinu ya usafiri na usafirishaji, maji, nishati, kilimo, mifugo, uvuvi, misitu, utalii, viwanda, biashara, uwezeshaji wananchi kiuchumi na miradi ya kimkakati.
Takwimu hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Martine Shigela hivi karibuni alipokuwa akizungumza mubashara na waandishi wa habari hivi karibuni wakati wa hitimisho la kipindi cha tumewasikia, tumewafikia katika ukumbi wa Ofisi ya Msemeji Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.
Mhe. Shigela ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amejielekeza katika kuwahudumia wananchi hususan wa vijijini huku akisema kuwa katika Mkoa wa Geita hakuna kata iliyokosa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Mkuu wa Mkoa wa Geita amefafanua kuwa ndani ya kipindi cha miaka minne viwanda vimeongezeka kutoka viwanda 824 mwaka 2021 hadi viwanda 1,542 mwaka 2025. Kadhalika utoaji wa leseni kwa wafanyabiashara umeongezeka kutoka leseni 1,346 mwaka 2021 hadi leseni 2,815 mwaka 2025.
“ Idadi ya vizimba vya kufugia samaki Mkoani Geita imeongezeka kutoka vizimba vinne mwaka 2021 hadi vizimba 27 mwaka 2025 na mitaji iliyotolewa na Serikali kwa wafugaji wa samaki imeongezeka kutoka shilingi Milioni 14 hadi Zaidi ya shilingi Milioni 792 kw mwaka 2025.” Aliongeza Mhe. Shigela.
Kwa upande wa Sekta ya Elimu Mhe. Shigela ameeleza kuwa hadi mwaka 2021 Mkoa ulikuwa na madarasa 7206 lakini hadi Juni 2025 Mkoa una madarasa Zaidi ya 10500 ikiwa ni ongezeko la asilimia 35 ambalo limesaidia kuwajengea wanafunzi kupata madarasa mengi ya kusomea na kujifunzia na kuondokana na msongamano wa wanafunzi darasani.
Akizungumzia upande wa Sekta ya Madini, Mkuu wa Mkoa wa Geita ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita inatambua kuwa sekta ya Madini ina nafasi ya kipekee katika uchangiaji wa pato la Taifa, upatikanaji wa fedha za kigeni na ukuaji wa uchumi kwa ujumla ambapo uzalishaji wa madini katika Mkoa wa Geita umeongezeka kutoka tani 18.21 mwaka 2021 hadi tani 27.43 mwaka 2025. Pia Serikali imeongeza utoaji wa Leseni kwa wachimbaji wadogo kutoka 900 mwaka 2021 hadi 9774 ikiwa ni ongezeko la asilimia 1000 ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kujikwamua kiuchumi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa