WANANCHI KATA ZA LUDETE, KAKUBILO WAMKOSHA RC GEITA UJENZI WA ZAHANATI NA MADARASA ACHANGIA TOFALI 2000, MIFUKO 420 YA SARUJI
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ameunga mkono jitihada za ujenzi wa Zahanati na Shule kata za Ludete na Kakubilo Halmashauri ya Geita kwa kuchangia matofali yenye thamani ya shilingi 2,400,000/= na kufanikisha harambee ya mifuko ya Saruji zaidi ya 420.
Mhandisi Robert Gabriel ameunga mkono jitihada za wananchi baada ya kutembelea kata hizo na kuridhishwa na kazi za ujenzi wa Zahanati za vijiji na Shule zinazofanywa na wananchi kwa kujitolea kufanya kazi bila malipo, kuchangia vifaa mbalimbali vya ujenzi na kuchimba misingi.
Akiwa Kata ya Ludete Mkuu wa Mkoa amesema " Nimefurahi sana kuona namna mnavyoshiriki katika utekelezaji wa miradi hii niwaombe mshiriki kuanzia mwanzo hadi mwisho na msikubali mtu yeyote kuwavunja moyo kwa kuwa maendeleo ya Ludete yataletwa na wananchi wenyewe hivyo mimi ninawachangia matofali 1000 kwa ajili ya Zahanati na mengine 1000 ya kujenga vyumba vya madarasa shule ya Sekondari Ludete".
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa Diwani wa Kata ya Ludete Sebastian Benedicto Mranda amesema kuwa wananchi wameamua kujitolea kushiriki ujenzi wa Shule mpya ya msingi baada ya shule ya Msingi Ludete kuwa na Idadi ya wanafunzi 6,616 huku kukiwa na madarasa 20 yenye mikondo 108 ambao unasababisha msongamano wa wanafunzi darasani. Marando ameongeza kusema kuwa Kata ya Ludete haina Zahanati kwa muda mrefu hivyo wananchi wamejihamasisha kujenga ili wapate huduma katika maeneo yaliyo jirani pia kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na Zahanati na shule ya msingi na Sekondari kwa Kata, Kata ya ludete ina wanafunzi 900 wanaotarajia kujiunga na elimu ya Sekondari ikiwa na uhaba wa zaidi ya vyumba vya madarasa 20.
Katika ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa amefanya harambee ambayo imefanikisha upatikanaji wa mifuko ya Saruji zaidi ya 420 na kuziagiza Halmashauri kutumia vikundi vya mafundi waliokatika maeneo ya miradi ili kupunguza gharama na kusimamia matumizi ya fedha za miradi hiyo.
Kutokana na Mkoa wa Geita kuwa na uhaba wa vyumba vya madarasa na Zahanati Serikali imeamua kushirikiana na wananchi kufanya kampeni ya mkoa mzima kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki na kuchangia ujenzi wa miradi ya maendeleo ili wananchi wapate huduma katika majengo bora na mazingira salama.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa