Mkuu wa Mkoa Geita akabidhi milioni 173.5 kwa Vikundi 26 vya Vijana na Wanawake
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, amekabidhi mkopo wenye thamani ya shilingi Milioni Mia Moja Sabini na Tatu na Laki Tano (Tshs.173,500,000) kwavikundi ishirini na sita (26) vyenye jumla ya wanachama Mia Tano Themanini na Tisa (589) ikiwa utekelezaji wa utoaji wa fedha asilimia kumi (10%) ya makusanyo ya ndani leo tarehe 22/05/2018 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Akiwasilisha taarifa kwa mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Geita, Bw. Ali A. Kidwaka alieleza kuwa, hadi sasa kwenye mpango na bajeti ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2017/2018, jumla ya Milioni Mia Mbili Ishirini (Tshs. 220,000,000/=) zimetolewa ikiwa ni asilimia kumi (10%) ya mapato ya ndani. Ambapo awamu ya kwanza, hadi kufikia tarehe 30, Aprili mwaka huu, Halmashauri imeweza kutoa jumla ya Tshs. 57,000,000 kwa vikundi 16 vya wanawake na vikundi 10 vya vijana.
Kwa upande wake mgeni rasmi Mhe. Mhandisi Gabriel alianza kwa kuwashukuru wanavikundi kwa mahudhurio yao mazuri na kuzidi kusisitiza Azma na Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuelekea Tanzania ya viwanda, kwa lengo la kumkomboa mwananchi maskini ili aweze kujishughulisha na kujiajiri yeye mwenyewe na kuwa na maisha bora. Alikemea migogoro ndani ya vikundi inayosababisha vikundi vingi kusambaratika baada ya kupewa mikopo hivyo kupelekea ucheleweshwaji wa mikopo kupitia msemo katika msafala wa Mamba, Kenge pia wamo.
Alimaliza kwa kusema “serikali kwa kupitia wataalam wake, haitaweza kufumbia macho vikundi vya aina hii na sheria kali itachukuliwa dhidi ya vikundi hivyo”. Lakini pia aliwakumbusha wanavikundi kwa msemo wa kijasiliamali usemao “mali bila daftari, hupotea bila habari” na kuwaomba wadau wa maendeleo na taasisi za kifedha kuendelea kutoa elimu ya utunzaji fedha, kisha kukabidhi mikopo hiyo.
Pongezi kwa ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kupitia, Idara ya Maendeleo ya Jamii, Timu ya Ukusanyaji wa Mapato, Kamati ya Mikopo, Wanasheria na Waheshimiwa Madiwani wote kwa pamoja katika kuhakikisha mapato yanakusanywa na asilimia 10 ya makusanyo inawafikia walengwa.
Miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, Wawakilishi wa NSSF, CCM, NHIF, NMB, TRA, LAPF na SIDO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa