MKUU WA MKOA ATEMBELEA HOSPITALI TEULE YA MKOA WA GEITA ASALIMIA WAGONJWA
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amefanya ziara katika Hospitali Teule ya Mkoa wa Geita ili kujionea hali ya utoaji wa huduma kwa Wananchi pamoja na kusalimia wagonjwa na kutambua mahitaji muhimu yaliyopo katika Hospitali hiyo.
Akiwa Hospitali hapo Mkuu wa Mkoa ametembelea na kukagua ujenzi wa wodi ya watoto wachanga (wenye umri chini ya siku 28) na watoto njiti (neonatal and Premature ward) ambayo ujenzi wake umefikia hatua ya lenta ikiwa na uwezo wa kuhudumia watoto 40, kutembelea wodi za wagonjwa, kukagua chumba cha X-Ray, chumba cha upasuaji, Stoo ya dawa, maabara, na chumba cha damu salama.
Mkuu wa Mkoa ameridhishwa na uwepo wa dawa za kutosha pamoja damu salama katika Hospitali hiyo, hata hivyo ameagiza ifanyike kampeni maalumu ya kukusanya damu ili kuwa na akiba ya kutosha kwa ajili ya kuhudumia wananchi wengi wakati wa matukio makubwa ya ajali.
Aidha, ameridhishwa na uwepo wa vitanda vingi vya wagonjwa vizima na vinavyohitaji matengenezo katika wodi na stoo, hivyo ameeleza kuwa Mkoa una kampeni ya ujenzi wa Zahanati 200 katika vijiji ambayo itaanza wiki ijayo. baada ya kukamirisha ujenzi vitanda vitatengenezwa na kupelekwa katika Zahanati hizo.
Mheshimiwa Robert Gabriel ametoa wito kwa wananchi kuwa na imani na Madaktari na wauguzi kwasababu ni wataalmu na wanajua kazi zao za kuhudumia wagonjwa kama kuna tatizo wasisite kutoa taarifa kwa uongozi. Hata, hivyo Mkuu wa Mkoa amewapongeza madaktari kwa kazi nzuri ya kutoa huduma kwa wananchi hivyo kuwataka wananchi kuwapa ushirikiano wakati wote wa kutekeleza majukumu yao.
Na:Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa