MKUU WA MKOA ATOA ONYO KWA VIONGOZI WANAOTUMIA MICHANGO YA WANANCHI KWA MASLAHI BINAFSI BUKOMBE
Viongozi wa vijiji, kata na tarafa Wilayani Bukombe wametakiwa kutumia michango inayotolewa na wananchi kwa shughuli zilizokusudiwa ili kuwaletea wananchi maendeleo katika maeneo yao.
Akizungumza katika kijiji cha Kazibizyo kata ya Ng'anzo Wilaya ya Bukombe Mhandisi Robert Gabriel Mkuu wa Mkoa wa Geita amesema katika vijiji, kata na tarafa wananchi wamekuwa wakihimizwa kujitolea kuchanga michango ya hiari ili kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo lakini baada ya michango hiyo kukusanywa inatumika kwa maslahi binafsi ya Viongozi.
Amesema kuwa Viongozi hao wasio na maadili wanapanga matumzi ya fedha za wananchi bila kujali vipaumbele vya vijiji kwa maslahi yao binafsi vitendo hivyo vinawavunja moyo wananchi wa kutoendelea kutoa michango ya maendeleo. "Kuna vidudu vinavyoleta magonjwa watu wanasubili maendeleo hayatokei inabidi tuvitoe tuvipige sindano kubwa vife humu humu viongozi wa namna hiyo wasio na maadili wamekuwa wakihamishwa wakati hawajatoa taarifa za mapato na matumizi alah! kama yupo Geita arudi arejeshe fedha za wananchi popote alipo".
Amesema kama kuna mtu au mtendaji anayeona hatoshi apishe akae pembeni ili wanaoweza kufanya kazi wafanye ili kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi. Hata hivyo, ametoa wito kwa wananchi kutumia rasilimali zinazowazunguka kujiletea maendeleo badala ya kukaa na kulalamika maisha magumu wakati kuna rasilimali nyingi katika maeneo wanayoishi. Aidha, amezitaka Halmashauri Mkoani Geita kusajili na kuvitumia vikundi vya mafundi vinavyojitolea kujenga madarasa na Zahanati bila malipo katika miradi ya fedha katika maeneo mbalimbali ili vijana hao wanufaike badala ya kutoa kazi zote kwa wakandarasi.
Awali Josephat Maganga Mkuu wa Wilaya ya Bukombe amemweleza Mkuu wa Mkoa kuwa Wilaya ya Bukombe ina vijiji 52 na Vitongoji 372 lakini kuna Zahanati sita (6) tu za Serikali. Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel akiwa Wilayani humo amezindua kampeni ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na Zahanati katika vijiji vya Kazibizyo na Bulama kwa kushiriki katika ujenzi na harambee iliyoleta michango ya mifuko 93 ya simenti, fedha tasilimu shilingi 340000/=, tofali 500,mbao 50 na misumari kilo3.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa