MKUU WA MKOA WA GEITA AZINDUA NA KUWEKA MAWE YA MSINGI KWENYE MIRADI SABA (7) YA MAENDELEO HALMASHAURI YA MJI GEITA
Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga amefanya ziara Halmashauri ya Mji wa Geita ambapo amezindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi Saba (7) ya Maendeleo.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amezindua vituo vitatu vya afya ambavyo ni kituo cha afya Mtakuja kilicho katika kata ya Mtakuja, Kituo cha afya Nyanguku kilichopokata ya Nyanguku na Kituo cha afya Shiloleli kilicho kata ya Shiloleli. Aidha, ameweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa shule mpya Tumaini shule msingi iliyopo Nyankumbu mjini Geita, Ujenzi wa madarasa manne na ofisi ya kidato cha tano, Ujenzi wa Mabweni ya wasichana na Bwalo la chakula Shule ya Sekondari Kasamwa.
Mkuu wa Mkoa amepongeza juhudi zinazofanywa na Halmashauri hiyo na kuwataka kuendeleza jitihada hizo katika maeneo mengine ya Halmashauri ili wananchi wapate huduma katika mazingira mazuri na kuwataka wananchi kushirikiana na Serikali yao bega kwa bega ili kuongeza kasi ya maendeleo.
Awali akielezea miradi hiyo Mhandisi Modest Aporinali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita amesema kwamba Halmashauri hiyo imetenga bajeti ya shilingi milioni mia moja na fedha hiyo ipo kwa kila mradi. Halmashauri ya Mji Geita ina mahitaji ya vituo kumi vya afya kwa sasa ina vituo viwili tu ambayo vinafanya kazi.Hata hivyo amesema Halmashauri hiyo inaendelea na jitihada za kutatua changamoto hiyo kwa kutumia mapato ya ndani na pia kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kama kampuni ya GGML ambayo imeahidi kiasi cha Shilingi milioni mia moja kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Mgusu.
Nao wananchi wamepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali kwa kusaidia kusogeza huduma karibu na maeneo yao kwa kuwa zamani walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Na. (Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita)
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa