MPANGO KABAMBE WA MAENDELEO YA MJI GEITA KUINUA UCHUMI WA MKOA
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amewataka wadau wa maendeleo ya Mkoa wa Geita kutumia fursa zinazopatikana katika mkoa huo na namna ya kuzitumia ili kuboresha maisha ya wananchi na kuinua uchumi kwa ujumla.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha kujadili mpango kabambe wa maendeleo ya Halmashauri ya Mji wa Geita 2017-2037 hivi karibuni katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji, Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa fursa kama uwepo wa eneo la kanda ya madini, mazi wa makuu, misitu ya asili, bonde lenye rutuba kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na barabara zinazounganisha mji huo na maeneo ya jirani zipangiwe mikakati itakayo wakwamua wananchi kiuchumi. “Mzingatie kuwa Halmashauri ya Mji Geita ndipo makao makuu ya Mkoa wa Geita na kitovu cha utawala na ukuaji wa uchumi wa mkoa ambapo shughuli zote za kiutawala, kijamii na kiuchumi zinafanyika, Hivyo Mpango kabambe ni muhimu kutekelezwa.” Aliongeza Mhandisi Robert Gabriel.
Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa mji wa Geita unatoa soko la mazao kwa shughuli zinazofanyika katika wilaya hii, shughuli za usafirishaji, utalii, utawala, afya, elimu na benki hivyo ni vema uhusiano uliopo ukajadiliwa kwa kina ili kuleta chachu ya maendeleo kwa miji na maeneo yote yanayozunguka mkoa kwa ujumla.
Akieleza umuhimu wa mpango huo Mkuu wa Mkoa wa Geita amefafanua kuwa endapo mpango huo utatekelezwa vizuri utapunguza kero za viwanda vinavyotoa hewa chafu ambavyo viko pamoja na makazi ya watu, sehemu za kuabudia pamoja na maeneo ya starehe na baa zilizojengwa katikati ya makazi ya watu.
Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Mji Geita Ndg. Oswald Cassian amesema kuwa mpango kabambe ni dira ya kuongoza, kusimamia na kudhibiti maendeleo ya ardhi kwenye sekta zote zinazotumia ardhi kama vile afya, elimu, barabara, maji, umeme, makazi/ viwanda na mengineyo. Mpango huo ulianza kuandaliwa na Halmashauri kwa kushirikiana na wataalam kutoka Wizara ya Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi mwaka 2014.
Mji wa Geita ni moja kati ya miji 18 inayofadhiliwa na mradi wa ULGSP chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia, ambapo mpango kabambe ni moja ya mradi unaofanyika chini ya mpango huo. Kauli mbiu ya mpango huoni “MPANGO KABAMBE WA MJI WA GEITA KATIKA KUSIMAMIA UENDELEZAJI WA RASLIMALI ZA MADINI YA DHAHABU”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa