Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 Ndugu Ismail Ali Ussi ameridhishwa na kutoa pongezi za dhati kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa ujenzi wa Ofisi bora na ya kisasa kwa ajili ya wataalam wa kada mbalimbali wanaofanya kazi katika Kata ya Bugulula.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ametoa pongezi hizo alipokuwa akizindua mradi wa Ofisi ya Kata ya Bugulula, Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita tarehe 1 Septemba 2025.
Ndg. Ismail Ali Ussi ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha wataalam wake wanapata mazingira rafiki ya ufanyaji kazi na wananchi wa kata zote Nchini wanapatiwa huduma za utatuzi wa changamoto mbalimbali katika maeneo ya jirani na makazi yao ndio sababu wakurugenzi wa Halmashauri zote wamesisitizwa kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za vijiji, mitaa na kata.
“Miaka ya nyuma ilikuwa ni ndoto kuona ofisi ya Serikali tena katika ngazi ya kata imejengwa kisasa na katika ubora wa hali ya juu utadhani hoteli, lakini Ofisi ya Kata ya Bugulula ambayo iko Geita vijijini imejengwa katika mfanano wa hoteli ya kisasa iliyopo mjini, hili ni jambo la kujivunia uongozi imara wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia nitoe pongezi za dhati kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kufanikisha ujenzi huu kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri.” Aliongeza Ndg. Ismail Ali Ussi.
Akitoa taarifa ya mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mtendaji wa Kata ya Bugulula Bw. Juma Gorwe Choma amesema kuwa ujenzi wa ofisi hiyo ulioanza mwezi Februari 2025 umetumia jumla ya shilingi Milioni 144,704,000/= ambapo kati ya fedha hizo shilingi 846,000/= zikiwa ni nguvu za wananchi wa Kata ya Bugulula.
Bw. Juma Choma ameeleza kuwa faida ya Ofisi hiyo ni pamoja na kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuwa huduma zote za kiutawala zitapatikana katika jengo moja, kadhalika mradi huo utatoa suluhisho na kupunguza gharama kwa kulipa kodi katika majengo ya watu binafsi walipokuwa wamepanga awali.
Ukiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mwenge wa Uhuru umetembelea, kufungua, kuzindua, kuweka mawe ya msingi na kukagua jumla ya miradi tisa yenye thamani ya shilingi za kitanzania Bilioni 2.8 ukiwa umebeba Kauli Mbiu isemayo “JITOKEZE KUSHIRIKI UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2025 KWA AMANI NA UTULIVU”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa