Na Boazi Mazigo - Geita RS
Katika hali ya furaha na moyo uliojawa tabasamu, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Geita wamefarijika na hatua ya maendeleo ya Mradi wa ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo-Busisi) lenye urefu wa Km.3 na barabara unganishi zenye urefu wa Km.1.66 kwa gharama ya shilingi bilioni 716.3 ambapo wameonesha kuridhishwa na hatua ya mradi huo kisha kumpongeza Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan na kumuombea dua na afya njema ili aendelee kuwatumikia watanzania.
Hayo yamejiri Septemba 8, 2023 wakati wajumbe halo walipozulu kwenye eneo linapojengwa daraja hilo (kigongo-busisi) na kutoa wito kwa wakazi wa Geita kujiandaa kutumia fursa ya uwepo wa daraja hilo lakini pia kuwasihi wataalam watanzania wanaosimamia ujenzi huo, kuhakikisha linakuwa na kiwango na ubora uliokusudiwa.
Akiongea kwa nyakati tofauti, mwenyekiti wa CCM Mkoa Geita Nicholaus Kasendamila alisema, "hakika mwenye macho aambiwi tazama. Tumshukuru na kumpongesa sana Rais wetu mpendwa, tumuombee kwa Mungu aendelee kuwa na hekima na busara na viongozi twende tukaisemee miradi hii wananchi waijue na kama CCM tunaunga mkono juhudi hizi kwa 100%".
Mwenyekiti Kasendamila aliongeza kuwa wajumbe hao walifika hapo kwa lengo la kuona, kujifunza na kisha kwenda kuisemea miradi ikiwemo wa daraja hilo kisha kumpongeza mhe.Martine Shigela, mkuu wa mkoa Geita kwa namna alivyo na ushirikiano, msikivu na mshauri kwenye chama.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa Geita Mhe.Martine Shigela alisema, ‘serikali imetekeleza, daraja hili ni mkombozi kwa maendeleo ya wananchi wetu. Tumshukuru sana mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwakuwa alipoingia madarakani, daraja hili lilikuwa kwenye 25% ya utekelezaji lakini hadi sasa lipo 76.34% kama tulivyoelezwa na mtaalam. Ajira nyingi zimepatikana kwa wazawa na wananchi anzeni maandalizi kutumia daraja hili kiuchumi".
Awali akitoa maelezo ya mradi, mhandisi William Sanga ambaye ni msimamizi wa mradi kutoka wakala wa barabara nchini TANROADS Mwanza alisema, mradi huo unafadhiliwa na serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania na muda wa utekelezaji ni miezi 48 kuanzia tarehe 25 februari, 2023 na hivyo unarajiwa kukamilika ifikapo Februari 24, 2023 wenye gharama ya Bilioni 716.3 na utakapokamilika utaondoa uwezekano wa kutokea vifo vinavyoweza kutokea kutokana na ajali za vyombo vya kuvukia eneo hilo. Vilevile alisema, muda wa kuvuka utakuwa ni dakika 4 kutoka zaidi ya Saa mbili za kupitia kwenye feri kwa sasa.
Mhandisi Sanga aliongeza kuwa, mradi huo mpaka sasa umetoa ajira 1,001 ambapo kati ya hizo, 944 zimetolewa kwa watanzania na 57 kwa raia wa kigeni na kwamba daraja hilo litakapokamilika litakuwa daraja la sita (6) katika Bara la Afrika likitanguliwa na madaraja ya 6th October Bridge (Misri) mita 20,500, Third Mainland Bridge (Nigeria) mita 11,800, Suez Canal Bridge (Misri) mita 3,900, Mozambique Island Bridge (Msumbiji) mita 3,800 na Dona Ana Bridge (Msumbiji) mita 3,670.
Ziara hiyo ilihitimishwa baada ya wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM Mkoa Geita kutembelea hospitali ya rufaa ya mkoa wa Geita, uwanja wa ndege Geita (Chato), stendi ya mabasi Kahumo, Bandari ya Nyamirembe, hospitali ya rufaa ya kanda chato pamoja na kuzulu katika kabuli la Hayati Dkt.John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa awamu ya Tano wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa