Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mhandisi Hamad Masauni (Mb) amekabidhi boti ya abiria wanne kama jitihada za kuimarisha ulinzi katika maeneo ya ziwa Victoria kwa ukanda wa Geita pamoja na kituo cha muda cha kikosi cha polisi Wanamaji wilayani Chato Mkoani Geita tarehe 13.08.2018
Mhe. Mhandisi Masauni ameanza kwa kuupongeza Mkoa wa Geita kupitia uongozi wa Mkuu wa Mkoa pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kusimamia amani na utulivu na kuifanya Geita iendelee kuwa tulivu na ya amani.
Amesema “wakati tunasubiri ujenzi wa kituo cha polisi wanamaji cha kudumu hapa Chato kitakachohudumia mkoa mzima wa Geita na maeneo jirani, leo tumeleta kituo cha muda kinachohamishika lakini pia nitawakabidhi boti moja ili kuanzia ninapoondoka hapa leo hiki kituo cha polisi wanamaji kianze mara moja hivyo mvitunze na kuvilinda”.
Ametoa wito kwa jeshi la polisi hasa kwa watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa visingizio na kukosa maadili kuhakikisha wanafanya doria kwa wakati utakaoelekezwa ili kuleta ufanisi wa kikosi hicho. Alionya baadhi ya askari wanaokiuka misingi ya kazi kwa kusema, “hii ni kwa nchi nzima, hatuwezi kuwaacha mapolisi wachache wakaharibu taswira ya jeshi kwa kuwepo matumizi ya nguvu yasiyo ya lazima kwa wananchi, ama kubambikia watu kesi na makosa yote ya uadilifu”, na kwamba askari atakayebainika amekiuka sheria, kanuni na taratibu, atachukuliwa hatua kali za kinidhamu. “Lengo la serikali ya awamu ya tano ni kuona wananchi wanatendewa haki, hivyo polisi wachache wasituharibie” alisema Mhe. Naibu Waziri.
Si hivyo tu, bali aliendelea kwa kusema, “msione kama vitendea kazi kwenu vinachelewaa, bali jueni ya kwamba umakini wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Rais wa kuhakikisha kodi za wananchi zinatumika kwa matumizi sahihi, na si kwa maslahi ya wachache wenye nia ya kujinufaisha wenyewe unazingatiwa. Tupo katika mapitio ya bei ili kupata thamani halisi ya fedha ya magari tuliyoagiza mia saba sabini na saba ambayo mengine yamekwisha ingia kwa kuwa kutokana na miktaba hovyo ya kifisadi, wastani wa bei ya gari moja ilikuwa ni sawa na magari matatu na serikali ya awamu hii tunasema hapana, vuteni subira tuokoe fedha ya watanzania”.
“Vivyo hivyo hata kwenye ujenzi wa nyumba elfu nne mia moja thelathini na sita nchi nzima ambapo nyumba moja iliwekewa thamani ya shilingi milioni mia mbili lakini za Arusha zilijengwa kwa fedha isiyozidi milioni ishirini na tano ambazo ndizo tunataka na si vinginevyo”. Alimaliza.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel akachukua fursa hiyo kumshukuru Mhe. Naibu Waziri kwa ujio wake kuikumbuka Geita upande wa ulinzi na usalama na kuongeza kuwa, tukio hilo linaongeza nguvu, na ulinzi zaidi kwenye mwambao wa ziwa Victoria ikiwemo kuzuia uvuvi haramu. Alishukuru pia uanzishaji wa kituo hicho cha polisi wanamaji kisha kuwaasa jeshi la polisi kuhakikisha kuwa vifaa vilivyokabidhiwa kwao vitatumika kwa lengo stahiki, na visitumike kusindikiza vitu haramu. Alisisitiza kuwa kama mkoa “hatutaficha uchafu, iwe taasisi ya aina yoyote ile, kila mmoja atomize wajibu wake” , kisha makabidhiano ya boti na kituo yakafanyika.
Miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita na viongozi wa CCM Wilaya ya Chato, Kamati za Ulinzi na Usalama Mkoa na Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Madiwani pamoja na wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa