Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) pamoja na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) wameendelea kupongezwa kwa jitihada wanazozifanya kupitia ushirikiano walionao kwa kubuni, kusimamia na kutekeleza mradi wa uendelezaji wa biashara kwa wajasiriamali wa mkoa wa Geita ambao umelenga katika kuwainua wananchi wa mkoa huo na taifa kiuchumi huku wakishirikiana na taasisi mbalimbali zinazotoa ujuzi kuweza kuwaimarisha katika shughuli wanazozifanya ikiwa ni azma ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na kiongozi shupavu Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha na kuongeza uchumi jumuishi nchini.
Pongezi hizo zimetolewa kwao leo januari 20, 2022 na mkuu wa mkoa wa Geita Mhe.Rosemary Senyamule wakati akifungua Warsha iliyoandaliwa kwa wajasiliamali na kufanyika katika ukumbi wa Sekondari ya Aloysius Mjini Geita huku akimshukuru mtendaji wa baraza la NEEC kwa jinsi ambavyo wameendelea kuwa karibu na mkoa huo wakihakikisha wananchi wanawezeshwa huku akiwahimiza wajasiriamali hao kuleta matokeo chanya baada ya kuwa wamepata mafunzo hayo ili kutumia fursa zinazopatikana ndani na nje ya Geita bila kuacha kuwahimiza wanaGeita kupenda kuwekeza nyumbani.
“niwashukuru NEEC kwa haya mnayoitendea Geita, nimshukuru mdhamini mkuu GGM kwa kuwezesha hili kufanyika na tutambue kuwa mhe.Rais anataka tuufikie uchumi wa juu na ndiyo maana NEEC wanajitahidi kuifanya idadi ya wazalishaji iwe juu tuweze kufikia lengo. Shime kwenu wajasiriamali, wekezeni kwenye maeneo mbalimbali, siyo eneo moja. Mafunzo mliyoyapata msiyatumie kwa ajili ya Mgodi wa GGM pekee bali hata migodi mingine na taasisi nyingine ndani na nje ya Geita. Vilevile ni muhimu wajasiriamali hawa wakasaidiwa kuchangamkia fursa zitokanazo na ujenzi wa bomba la mafuta linalopita mkoani kwetu lakini mnapofanikiwa msisahau kuwekeza nyumbani, yaani vuna Geita, wekeza Geita”, alisema mhe.Senyamule.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bibi. Beng’i Issa katika taarifa yake amesema kuwa, “kwanza naupongeza mgodi wa GGM kwa ufadhili wa mradi huu uliopo hatua za majaribio ambao umewezesha upatikanaji wa mafunzo ya usimamizi wa biashara kwa watu 365 awamu ya kwanza, elimu nadharia kuhusu uundaji wa umuhimu wa kongano za biashara kwa watu 117 na awamu ya tatu ya mafunzo ya vitendo yaliyotolewa na SIDO yaliyohusisha wajasiriamali 109. Katika awamu ya nne wajasiriamali 131 walishiriki mafunzo na kuunda kongano, na awamu ya tano ya malezi ya biashara yaliyowahusisha kukutanishwa wajasiriamali wadogo 101 na wafanyabiashara wakubwa 37 ili kuwasaidia wajasiriamali wakue”.
“hadi kufikia tarehe 31 desemba, 2021, kituo kimefanikiwa kuhudumia jumla ya wananchi 452 wanawake wakiwa 167 na wanaume wakiwa 285 kati yao. Vilevile, jumla ya shilingi milioni mia mbili na mbili (202,000,000) zilitolewa kama mkopo kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wa SELF Microfinance lakini pia kituo kimeweza kuunganisha wafanyabiashara 54 ili kufanya kazi na mgodi ambapo mpaka sasa wafanyabishara 15 wamesajiliwa na mgodi, 8 wapo kwenye mapitio ya mwisho, na 2 wanaendelea na usajili kwenye kanzi data”, aliongeza bibi Beng’i.
Mwakilishi wa GGML bw.Reward Tenga uwezeshaji huo ni moja ya tunu zinazosimamiwa na mgodi huo na ndiyo maana pamoja utoaji wa fedha za wajibu wa kampuni kwa jamii yaani CSR bao wako bega kwa bega kuhakikisha wanashiriki kuhakikisha maisha ya wana Geita yanainuka.
Mwisho, mkuu wa wilaya ya Geita mhe.Wilson Shimo ametoa rai kwa wajasiriamali kusaidiana, kushirikishana, kujengeana uwezo wenyewe kwa wenyewe yaani wakubwa kwa wakati, wakati kwa wadogo ili kwa pamoja kuleta mafanikio na kisha kusisitiza juu ya watanzania kuja na kuwekeza wilaya ya Geita lakini pia wajasiriamali kuwa na matokeo chanya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa