Katika mwendelezo wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Katibu Tawala Mkoa wa Geita Bw. Denis Bandisa ameendelea kutekeleza programu iliyoandaliwa na mkoa huu ya namna ya kuadhimisha wiki hii, kwa kukutana na kufanya kikao na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Geita Mji katika Ukumbi wa Mikutano wa GEDECO uliyopo Halmashauri ya Mji Geita juni 21, 2019
Akizungumza kwa nyakati tofauti, Bw. Bandisa amewaasa watumishi wa umma, juu ya kuwa na nidhamu kazini, kuwa wawazi na wawajibikaji wakitambua kuwa, hakuna haki bila wajibu wanapotekeleza majukumu yao lakini pia ushirikiano baina yao ndiyo utakaoleta matokeo chanya huku akiwapa kanuni ya “TAPE” kama kifaa muhimu kitakachoivusha taasisi.
Amesema, “watumishi wa umma, ni vyema mtambue majukumu yenu kwa mujibu wa mkataba, muwe na mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli zenu za kila siku. Wenye kasoro mjirekebishe, tujenge mahusiano mema kazini, lakini vile vile tuwe mabalozi wa kuelimisha wananchi juu ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliyopo mbele yetu ili waitumie haki hiyo kikamilifu. Ningependa mtumie kanuni ya TAPE katika kufanya kazi zenu, mtafanikiwa”.
Bw. Bandisa ametoa tafsiri ya neno TAPE akimaanisha T-Transparency yaani (Uwazi), A-Accountability yaani (Uwajibikaji), P-Participation yaani (Ushirikishwaji) na E-Equity yaani (Usawa), ikiwa na maana kuwa, wakuu wa idara na vitengo wana wajibu wa kushirikiana na watumishi wengine kufanya kazi uwazi, ushirikishwaji, usawa na uwajibikaji na kuwasihi kukusanya mapato pamoja na kuwa na miradi ya kimkakati ya kiuchumi.
Awali katika kikao hicho, Meneja wa Mkoa wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bw. Odhiambo Elius, aliweza kuongea na watumishi hao akikusanya maoni na changamoto zinazowakabili huku akitoa fafanuzi za masuala mbalimbali yaliyoulizwa na kuwasihi watumishi kuwashawishi ndugu, jamaa na marafiki ambao ni wakulima kujiunga na Mpango Maalum wa Bima ya Afya kwa Wakulima Walio Katika Vyama vya Ushirika wa Mazao (AMCOS) ujulikanao kama “Ushirika Afya” , mpango utakaowawezesha kupata huduma za afya.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wakuu wa idara mbalimbali na vitengo kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa geita, wawakilishi wa wakurugenzi wa halmashauri hizo bila kusahau watumishi wa ngazi zote wa halmashauri zote mbili.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa