Katibu Tawala Mkoa wa Geita Bw. Denis I. Bandisa amesema yupo Mkoani Geita kwa lengo la kufanikisha shughuli zote za maendeleo bila kupendelea upande wowote.
Amesema kauli hiyo tarehe 01.11.2018 wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita kufuatia Madiwani hao kutokuwa na uelewa juu ya maelekezo yaliyokuwa yametolewa kwenye kikao cha baraza hilo awali tarehe 27.10.2018 juu ya upandishwaji hadhi kituo cha Afya Nzera kuwa Hospitali ya Wilaya kilichopo Jimbo la Geita, jambo lililopelekea fedha kiasi cha Shilingi Bilioni Moja, Milioni Mia Tano kuelekezwa sasa kwenye Hospitali ya Wilaya Nzera.
Akitoa ufafanuzi wa suala hilo Bw.Bandisa alianza kwa kusema, “wahe. Madiwani, tambueni ya kuwa, nimeteuliwa kuja kuisaidia Geita isonge mbele kimaendeleo bila upendeleo wa mahali popote, hivyo niwaombe mpendane, mshikamane, muwe kitu kimoja kwenye suala zima la maendeleo lakini pia kama kuna jambo mnahitaji ushauri basi msisite kufika ofisini niko tayari kuwasaidia”.
Bw. Bandisa amewaelekeza Madiwani hao kuwa, wanapaswa kutambua kwamba Serikali inaendeshwa kwa mujibu wa Sheria, Taratibu na Kanuni hivyo basi kama kuna jambo halijaeleweka ama kukubaliwa ni vyema kufuata njia sahihi kutatua changamoto ili kwenda pamoja kwakuwa nia ni kujenga akiwahakikishia kuwa Kituo cha Afya Katoro kitaendelea kuboreshwa lakini pia kampeni ya ujenzi wa zahanati kila kijiji, kituo cha Afya kila kata vitakua ni suluhu ya muda mrefu na vitapunguza msongamano kwenye Hospitali za Rufaa. Pia amewashauri wajumbe wa Baraza hilo kujenga hoja kwa kutumia fursa na changamoto wanazokumbana nazo na si kupingana na maagizo na maelekezo ya Serikali yanapokuwa yametolewa.
Mbunge wa Jimbo la Busanda Mhe. Lolesia Bukwimba, awali hakuwa amekubaliana na fedha hizo kupelekwa Hospitali ya Nzera lakini baada ya ufafanuzi uliyotolewa na Katibu Tawala ilionekana ni vyema kuwa na mbadala kutokana na ukweli kuwa bado kuna uhitaji wa kuwa na Hospitali yenye hadhi ya Wilaya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro kulingana na idadi ya watu waliyopo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe. Elisha Lupuga amewashukuru wajumbe hao kwa ukubali wao juu ya maagizo ya Serikali huku akisisitiza kuwa wamoja, wenye kuheshimiana na kupendana wakitambua kuwa jambo linapofanyika jimbo mojawapo basi ni kwa nia ile ile ya kuleta maendeleo na si vinginevyo. Amewashauri pia kutumia uzoefu wa Katibu Tawala Mkoa ili kufanikisha mipango yao kwakuwa anaamini kuwa mtumishi huyo ameletwa Geita si kwa bahati mbaya bali ni msaada muhimu sana wamtumie. Kisha Mwenyekiti Lupuga akawasamehe wajumbe ambao awali alitaka kuwapeleka kwenye kamati ya maadili vilevile akawataka Madiwani wote kwenda kufanya mikutano na Kamati za Maendeleo za Kata (WDC) ili kuona ni miradi gani itatekelezwa na fedha za Miradi ya Jamii (CSR).
Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Josephat Maganga amewaeleza wajumbe wa Baraza hilo kuwa, matatizo yapo pande zote yaani jimbo la Busanda na Geita kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina majimbo mawili hivyo kuchelewesha maamuzi ni kuchelewesha maendeleo lakini pia kupoteza rasilimali fedha na muda.
Mwisho Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bw. Ali Kidwaka akawasihi Wahe.Madiwani kutopenda kuwa na migogoro ndani ya Halmashauri kwani inachelewesha maendeleo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa