Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Geita afurahishwa na Ujenzi wa Shule ya Ghorofa ya Sekondari Nyalwanzaja Wilayani Geita ambayo kwa uwepo wake itaondoa adha kwa wanafunzi kutembea zaidi ya KM 14 kufuata Elimu hiyo, mradi unaoambatana na Ujenzi wa nyumba pacha ya walimu pamoja na matundu kumi ya vyoo na kugharimu zaidi ya Milioni 200.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema hayo tarehe 12, 04, 2021 wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Nyalwanzaja mara baada ya kuweka jiwe la Msingi kwenye Mradi wa Ujenzi wa shule ya Sekondari Nyalwanzaja iliyoasisiwa ujenzi wake na wananchi.
"Hii itakua shule ya kwanza ya Ghorofa Geita, nawapongeza sana wananchi wa hapa maana maendeleo haya ni ninyi ndio mmeyachochea." Amesema Mkuu wa Mkoa.
Akizungumza na viongozi wa shule mpya ya Sekondari Buyagu yenye wanafunzi wa kidato cha kwanza pekee, Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema ameridhishwa na matumizi ya fedha kwenye Mradi huo ambao hadi sasa umetumia fedha.Tshs. Milioni 90 na tayari wameshajenga madarasa 5, Ofisi 2 za walimu na matundu 8 ya vyoo na madarasa mengine mawili yakiwa kwenye hatua ya boma.
Aidha, Mhe. Mkuu wa Mkoa amewataka watendaji kwenye ngazi zote kujituma na kufanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha wanatatua kero za wananchi na kukamilisha Miradi kwa wakati huku akitoa rai kukamilisha ujenzi wa shule ya Sekondari Nyalwanzaja ukamilike ifikapo mwenzi Mei 2021.
Vilevile, Mhe. Mkuu wa Mkoa ametembelea Ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Nyabulolo na Kamena ambazo ziko kwenye hatua za mwisho kukamilisha na ameagiza ukamilishaji wa haraka ili huduma za mama na mtoto, wagonjwa wa nje, Afya ya uzazi, ziweze kutolewa kuanzia mwezi mei mwaka huu huku akitolea mfano wa unafuu mkubwa utaoletwa kwa zaidi ya wananchi 7786 kutoka Kamena waliokua wakitembea kilomita 15 kwenda kupata huduma hiyo.
Shule ya Sekondari Nyamalimbe yenye ziada ya vyumba vya madarasa 7 imemfurahisha Mhe. Mkuu wa Mkoa na amewapongeza uongozi wa Wilaya hiyo pamoja na shule kwa kujitoa kuhakikisha wanaondoa kero ya vyumba vya madarasa. Aidha, ameagiza ukamilishaji wa utengenezaji wa viti na meza vichache kwenye shule hiyo ili kuwapa wanafunzi mazingira mazuri ya kujifunzia.
Wakati huohuo Mhe. Mkuu wa Mkoa amesikitishwa na upungufu wa samani hasa kwenye maabara na upungufu mkubwa wa nyumba za walimu na mabweni ya wanafunzi wa kike kwenye Shule ya Sekondari Butobela na kaagiza ndani ya mwezi viongozi kwenye kata hiyo na wilaya waketi na kupate mkakati wa kukamilisha miundombinu hiyo.
Aidha, amehuzunishwa na matokeo dhaifu ya kitaaluma kwa kidato cha nne kwenye shule hiyo iliyoshika nafasi ya mwisho 2020 na akaagiza uthibiti ubora wa shule kumpatia taarifa ya kina ya sababu ya kufeli na akaagiza Katibu Tawala wa Mkoa kubadilisha Mkuu wa shule hiyo Mara moja kwa kushindwa kumudu majukumu yake.
"Yaani shule inakua ya mwisho mara mbili, ukipambana unabaki palepale, hii sio sawa Kaimu Katibu Tawala lete Mkuu wa shule mwingine apa ndani ya siku tatu awe amepatikana."
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Geita amehitimisha siku ya kwanza ya ziara yake wilayani Geita kwa kutembelea shule za Sekondari za Nyamalimbe, Butobela na Bukoli.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa