Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel kipekee ameendelea kukonga nyoyo za Watanzania kwa kuongeza furaha na tumaini jipya kwa washiriki wa maadhimisho ya Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima (NaneNane) Kanda ya Ziwa Magharibi inayojumusha mikoa ya Kagera, Geita na Mwanza ambayo yamefanyika katika viwanja vya Nyamhongolo vilivyopo Jijini Mwanza tarehe 08.08.2018 akiwa kama Mgeni Rasmi alipotangaza kuanzisha mkakakati wa ujenzi wa vibanda vya kudumu vya maonesho lakini pia kukubali ombi lakuongeza siku mbili baada ya kufunga maonesho ili wakulima waweze kufaidika zaidi na maonesho hayo yenye kauli mbiu isemayo “ Wekeza Katika Kilimo Mifugo na Uvuvi kwa Maendeleo ya Viwanda”.
Pamoja na mapokezi ya vikundi vya ngoma na kucheza na nyoka, Mhandisi Gabriel ametembelea mabanda yaliyoandaliwa vizuri yakiwa na wataalamu wanaotumia teknolojia mbalilmbali za kilimo na kujionea jinsi Tanzania ya Viwanda ilivyo mbioni kutimia. Ameelekeza zoezi la kuhakikisha eneo hilo la maonesho linalindwa na kujengwa rasmi kwa ajili ya maonesho, ambapo hata baada ya maonesho shughuli zinaweza kuendelea wananchi wakaendelea kujifunza. Pia ameshukuru kamati ya maandalizi na uongozi wa Mkoa wa Mwanza kwa mapokezi mazuri kwakuwa maonesho yamekuwa na watu wengi mno kiasi cha kwamba hata barabara zimepitika kwa tabu lakini pia yamependeza.
Amesema, “nia ya maonesho haya ni kuleta mapinduzi ya teknolojia ya kilimo, ili mkulima ajue namna ya kutumia vyema kanuni bora za kilimo ili kupitia eneo dogo azalishe kingi, yaani kuzalisha kibiashara na kuachana na kilimo cha mazoea, huku ni kuunga juhudi za Mhe. Rais za kukuza uchumi ambao unaambatana na uchumi wa viwanda kwani kilimo ni kiwanda cha malighafi”. Akasema pia gharama mikoa yote iliyoitumia kushiriki ioneshe matokeo, “hivyo hii iwe ni sehemu ya watu kuja kujifunza hata kwa mwaka mzima, isiachwe pakawa ni pori” aliongeza. Aliieleza Sekretarieti ya Mkoa kwa Kushirikiana na Kamati ya Maandali kuwa na mpango unaotekelezeka wa kujenga mabanda ya kudumu ili maonesho yafanyike hata mara tatu.
Ameshauri pia uanzishwaji wa Benki za Matofali ambayo yataweza kuhamasisha ujenzi wa haraka wa vindanda hivyo vya kudumu na kusema kama mwakilishi wa Mkoa wa Geita yupo tayari kushiriki ujenzi huo na kuungwa mkono na mikoa washiriki wa Mwanza na Kagera. Mhandisi Gabriel alifurahia kuona vitu mbalimbali vikiwemo Asali, Mashine ya Kulelea Vifaranga vya Kuku, Viatu,Ngozi ya Samaki, Ufugaji Samaki, Majiko, Matunda, Nyumba za Kijani (green houses),n.k
Aliweza pia kukabidhi zawadi za vikombe, vyeti pamoja na fedha taslimu kwa washindi washiriki wa maonesho hayo waliofanya vizuri kwenye vipengele tofauti wakiwemo RIJK-ZWAAN na KIBO Seed Co. Ltd Kampuni za Utengenezaji na Uuzaji wa Pembejeo za Kilimo,Vodacom Kampuni ya Mawasiliano, na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo mshindi wa kwanza ilikua ni Manispaa ya Ilemela Jijini Manza, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale iliyopo Mkoa wa Geita na ya tatu ikiwa ni Halmashuri ya Wilaya ya Misungwi ya Jijini Mwanza.
Naye mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe.Dkt. Severine Lalika alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Geita na Mgeni Rasmi kwa kukubali kufunga maonesho hayo kwa niaba ya washiriki na kuhaidi kutekeleza yale yote yaliyoelekezwa kwao kupitia hotuba yake.
Sherehe hiyo ilihudhuliwa pia na viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi n.k
Mkuu wa Mkoa wa Geita anaendelea kuwakaribisha kushiriki Jukwaa la Fursa za Biashara litakalofanyika Mkoani Geita kwa kushirikiana na Kampuni ya Magazeti ya Serikali TSN kuanzia tarehe 15-16.08.2018, nyote mnakaribishwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa