Katika kuhakikisha Halmshauri zote za mkoa wa geita zinapata hati safi, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ameendesha mkutano maalum wa baraza la madiwani kujadili hoja za mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2017/2018 (hoja zilizosababisha halmashauri hiyo kupata hati chafu), mkutano uliokuwa na matokeo chanya baada ya wajumbe wa mkutano huo kunuia kupata hati safi kwa miaka baada ya mwaka huo wa fedha walipoketi julai 16, 2019 katika ukumbi wa mikutano, halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale.
Akiongea kabla ya kuweka kikao wazi, mwenyekiti wa mkutano mhandisi Robert Gabriel amewaeleza wajumbe hao kuwa, kikao hicho ni muhimu na cha kipekee kwani kitatoa njia na mwelekeo sahihi wa kuondokana na hati isiyo safi na kisha baada ya majadiliano kuwapongeza wajumbe kwa michango inayoashiria kuwa wamejipanga kupata hati safi akisema kutenda kosa si kosa bali kurudia kosa.
“leo mmedhihirisha sasa tunaanza safari ya mabadiliko, lakini ni muhimu tuwe wawazi kwa fedha yoyote inayoingia ili kuwe na uelewa wa pamoja baina ya wataalam na madiwani. Vilevile mkaguzi wa ndani anatakiwa kutoa taarifa mara moja kupitia taarifa ya robo kila aonapo viashiria vya hoja ili tuidhibiti mapema, hivyo nitoe rai ya upatikanaji wa majibu ya hoja 44 zilizobaki kati ya 66 ndani ya wiki 2 na tujipange kuepuka hati chafu” amesema mhandisi Gabriel.
Taarifa ya mkaguzi wa ndani kuwasilishwa kwa madiwani kila robo pamoja na ukusanyaji wa mapato ili kuiwezesha taasisi hiyo kujiendeshe ikawa ni agizo kwa halmshauri hiyo.
Utunzaji wa nyaraka na uwazi vimekuwa ombi la wajumbe wengi, jambo lililopelekea mhandisi Gabriel kusisitiza watumishi kutunza nyaraka na kuwa wawazi wakishirikiana kisha kumpongeza mbunge wa jimbo hilo Hussein Amar kwa kujitolea kuleta maendeleo nyang’hwale hata kwa fedha zake binafsi.
Mbunge wa Nyang’hwale Hussein Amar kwa upande wake amesema, usiri ndiyo changamoto ya matatizo mengi hivyo ni vyema kuwa wawazi huku akiomba RC Gabriel kumfikishia ombi Mhe.Rais Magufuli kufanya ziara jimboni kwake ikiwa wananchi wanayo shahuku ya kutembelewa na kiongozi huyo
Katibu tawala mkoa Denis Bandisa yeye amewaeleza wajumbe kuwa, ili kutoka hapo walipo, wanahitaji kushirikiana na kusaidian kuanzia menejimenti ya halmashauri pamoja na watumishi bila kusahau madiwani ili kuiondoa kero ya hati isiyosafi.
Mustafa Mwangaile Kwaniaba ya Mkaguzi wa Nje Geita katika taarifa yake amesema, hoja 44 ambazo hazijapata majibu kati ya 66 zimegawanyika katika makundi manne kama vile, kutowasilishwa kwa hati za malipo, kuhamishwa kwa fedha bila kuonekana matumizi, upotevu wa vitabu vya kukusanyia mapato pamoja na malipo yaliyofanyika bila nyaraka kuwasilishwa.
Mkuu wa wilaya hiyo Hamim Gwiyama amewataka watumishi kujitathmini kwa kuhakikisha hawarudii makosa yaliyofanywa na watangulizi katika nafasi walizonazo akisema, hati hiyo isiyosafi imepatikana kutokana kukosa uadilifu, uwazi, utawala bora, uzalendo, ushirikishwaji, uwajibijaki n.k huku akitoa uzoefu wake akisema “uhasibu hauna siasa, nimekuwa mhasibu kwa miaka 20 sikuwahi kupata hati chafu bali safi wakati wote, hivyo jitathiminini kwenye hayo maeneo mtavuka” kisha kuwaasa kufuata maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa na sekretarieti ya mkoa.
Kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri hiyo Mariam Chaurembo amesema, wao wamejipanga na kwa sasa miradi mingi inakwenda kwa kasi ya kuridhisha ikiwemo ujenzi wa hospitali ya wilaya uliyo katika zaidi ya 70% ya utekelezaji, ujenzi wa maboma ya shule ya msingi 9 kwenye kata 10 na maboma mwengine 21 yakiwa na 95% kwa kuzingatia thamani ya fedha huku akishukuru ushirikiano kutoka ofisi ya katibu tawala mkoa wa geita.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Isack John kwaniaba ya halmashauri akamuahidi RC Gabriel kuyafanyia kazi yote yaliyoelekezwa na kwamba mwaka huu watapata hati iliyo safi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa