Ni jumatano angavu ya terehe 06.12.2018 iliyobarikiwa kwa hali nzuri ya hewa, ndipo Padri Thomas Kabika Bilingi, Chapleini wa Hospitali ya Sengerema anakanyaga malango ya ofisi ya mkuu wa mkoa wa geita.
Baada ya kufika na kupokelewa, ndipo alipoeleza nia ya ujio wake akisema “leo nimekuja kutimiza ahadi yangu kwa Mhe.Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Geita niliyoitoa wakati wa Kumzika marehemu dada wa Mhe. Constantine Kanyasu mwezi Agosti, 2018 katika kijiji cha Nyamboge Halmashauri ya Wilaya ya Geita. Nimeleta miche ya mikwaju elfu moja mia mbili (1,200) itakayogawiwa kwa Halmashauri zote Sita (6) kwa maana ya miche mia mbili (200) kwa kila Halmashauri”.
Ameeleza kuwa, kutoa miche ya miti hiyo kwa kisukuma ikiitwa “mishishi” na Kizinza “misisa”imekuwa ni desturi yake kila anapohudumu kwenye mazishi na kila anapofungisha ndoa huku akihamasisha miche hiyo itunzwe, ikuzwe kwaajili ya dawa, chakula (Sharubati) na utunzanji wa mazingira. Vilevile, Padri huyu anatoa miche hiyo kwakuwa amezaliwa kwenye kijiji kiitwachwo “Kasisa” (mane yake kuna mishishi mingi) kilichopo Halmashauri ya Buchosa ambapo miti hiyo hupatikana kwa wingi.
Amesema, miche hiyo hutoa matunda baada ya miaka nane (8) na ni mizuri haiharibiki hovyo na kwamba bado anayo hazina ya kutosha akisema ataendelea kuipanda miti hiyo hadi umauti utakapomkuta.
Ameeleza kuwa, bado anaendelea kuotesha miti hiyo na anayo mingi na kwamba baada ya kuona miti hiyo inafyekwa sana na watu akaona ni vyema aingie kwenye shughuli ya utunzaji mazingira, ni tangu aadhimishe miaka arobaini (40) ya Upadre na miaka hamsini na tano (55) ya Ubatizo wake katika miaka sitini (60) ya parokia mwaka 2017.
Akipokea miche ya miti hiyo kwa niaba ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Bw.Deodatus Kayango ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu amemshukuru Padri Bilingi kwa kutimiza ahadi yake na kwamba atahakikisha kila halmshauri inapata miche ya miti hiyo kama ilivyotarajiwa huku akiahidi kufikisha taarifa hiyo kwa Mhe. Mhandisi Gabriel.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kipekee inatoa shukrani za dhati kwa Padri Bilingi kwa kuwa kiongozi wa dini anayeenenda kwa mfano kupitia kitendo chake cha kutimiza ahadi aliyoitoa mwenyewe.
“Tukumbuke kuwa, Padri Bilingi amefanya kazi ya utunzaji wa mazingira kwa kugawa miche ya miti mingine tofauti na mikwaju tangu mwaka 1978 alipohudumu katika maeneo mbalimbali yakiwemo Bugando - Mwanza, Musoma, Nyarubele n.k”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa