Na Boazi Mazigo - Geita
Shirika lisilo la kiserikali la Plan International tawi la Geita kupitia Mradi wa Kuwezesha Wasichana Kuendelea na Masomo (KAGIS) katika kuunga mkono juhudi za serikali, limetoa jumla ya vitabu 52,683, vifaa vya michezo pamoja na vifaa vya kujifunzia kwa watoto wenye ulemavu kwa mikoa ya Geita na Kigoma vyote vikiwa na thamani ya Sh.438,289,448.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi ugawaji wa vitabu hivyo uliofanyika Agosti 30, 2022 katika eneo la Shule ya Msingi Mkoani, Mkuu wa Mkoa Geita Mhe.Martin Shigela ameipongeza Plan International kwa kuwa miongoni mwa wadau wenye mchango mkubwa kwenye sekta ya elimu akiwaomba kufikisha shukrani kwa serikali ya Canada na kuwaagiza viongozi mkoani Geita kuhakikisha kuwa vitabu na vifaa hivyo vinatunzwa na kutumika kwa makusudio husika.
Mhe. Shigela amesema, “niwapongeze Plan International kupitia mradi huu wa KAGIS na kwa kufanya hivi mnatekeleza malengo ya Milenia kumpatia elimu mtoto wa kike na kwamba kwa kuelimisha mwanamke unakuwa umeelimisha jamii kubwa ukizingatia kuwa mwanamke ni mchumi namba moja anapowezeshwa”
Vilevile, Mhe. Shigela amesema, ni vyema vitabu hivyo vikatunzwa na kutumika kwa usahihi huku akiipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya elimu bila malipo kutoka bilioni 20 mpaka bilioni 25 bila kuacha ujenzi wa shule mpya kwenye kila jimbo kupitia mradi wa SEQUIP kwa gharama ya milioni 470 na kwamba ni marufuku kwa watoto kuzuiwa kwenda shule kutokana na michago.
Amemaliza kwa kupongeza zoezi la sensa ya watu na makazi akiwashukuru kuanzia mratibu, wakuu wa wilaya, wakurugenzi, makarani mpka wenyeviti wa vitongoji kwa mkoa wa Geita na kusema, “mkoa wetu umevuka lengo kwa kuhesabu watu kwa 123% , lakini viongozi wa Mitaa na vijiji tusaidiane yule ambaye hajahesabiwa tupate majina kamili ili nao wahesabiwe ikiwa hawakuhesabiwa”
Akisoma taarifa ya mradi Bw.Nickodemus Gachu ambaye ni Mkurugenzi wa mradi wa KAGIS amesema wanafanya hivyo ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita kwa kutambua changamoto zinazoikumba sekta ya elimu hususan kwa watoto wa kike na ndiyo sababu Plan International kupitia ufadhili wa Serikali ya Watu wa Canada (CAG) kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania hufanya kazi kwa pamoja kukabiliana na changamoto hizo.
Bw.Gachu ameongeza kuwa, kupitia mradi wa KAGIS, chini ya ufadhili wa serikali ya Canada, jumla ya vyoo 50 vitajengwa katika shule za mradi kwa mikoa ya Geita na Kigoma, na kwa kipindi cha miaka mitano, mradi huo utawezesha ununuzi na usambazaji wa Baiskeli 2,220 kwa watoto wa kike wanaolazimika kutembea umbali mrefu akisema KAGIS “Muwezeshe Asome, Afikie Malengo”
Kwa upande mwingine, Katibu Tawala Mkoa Geita Prof.Godius Kahyarara amesema “vitabu ni mwalimu. Hivyo basi, wananfunzi ni vyema mvisome, msivichane kwani elimu ndiyo mkombozi wa kila kitu na mkoa upo tayari kutoa ushirikiano ili kufanikisha mambo mema ambayo Plan International inaufanyia mkoa wa Geita”
Baada ya salamu za pongezi kutoka kwa Mkuu wa Wilaya Geita Mhe.Wilson Shimo, mwalimu Albert Mugyabuso amabye ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi mkoani ameishukuru Plan International kwaniaba ya walimu wa shule zinazonufaika na mradi wa KAGIS akiahidi kutunza vitabu hivyo ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu na kwamba vitawanufaisha na wanafunzi wengine watakaokuja na kuwakaribisha wadau mbalimbali kuendelea kusaidia mahitaji katika maeneo mengine upande wa elimu.
Vitabu vilivyotolewa ni vya masomo ya Hisabati, Sayansi, Kiswahili na Kiingereza kwa darasa la nne mpaka la saba na vya kusoma, kuandika, kuhesabu, hadithi kwa darasa la kwanza na la pili na kwa mkoa wa Geita, vitabu na vifaa tolewa ni kwa shule 47 kutoka wilaya ya Geita yenye halmashauri za mji na wilaya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa