Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Tanzania aongoza watanzania kwenye Maziko ya Hayati Rais John Pombe Magufuli yaliyofanyika leo ijumaa tarehe 26, 03, 2021 wilayani Chato kwenye makaburi ya familia kwenye kijiji cha Mlimani.
Mhe. Rais ametoa shukrani kwa makundi mbalimbali kwa umoja na ushirikiano wakati wote wa msiba mzito wa Hayati JPM uliotokea Machi 17, 2021 kwa ugonjwa wa Moyo. Aidha, ametoa pole kwa familia ya Hayati Magufuli na ameahidi kuendelea kushirikiana nao na wanachato wote.
Naye, Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amewashukuru watanzania kwa utulivu na umoja kwenye kipindi cha Majonzi na wote walioshiriki shughuli mbalimbali za kufanikisha shughuli za kuaga na mazishi ya Hayati JPM na amewasihi kuendelea kushikamana.
Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Jobu Ndugai amemhakikishia Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu ushirikiano kutoka kwenye ofisi yake wakati wote katika kuhakikisha nchi yetu inafanikiwa na kusonga mbele zaidi kimaendeleo.
Jaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania Prof. Ibrahim Juma amesema Mahakama nchini itamkumbuka Hayati Magufuli kwa upendo wa dhati kwa watanzania Wanyonge nchini kwani alitamani watoke pale walipo na kuinuka kiuchumi na kiu ya kutaka mahakama nchini kubadilika ili kuendana na matakwa ya karne ya 21.
Dkt. Ally Mohamed Shein Rais Mstaafu wa awamu ya Saba Zanzibar amesema atamkumbuka Hayati JPM kwa ukweli na uungwana wake na kuthubutu kwenye mambo makubwa kila alipotaka litimie alihakikisha linakamilika kwa maslahi ya watanzania.
Mhe. Jakaya Kikwete Rais Mstaafu wa Tanzania amesema yeye na Hayati JPM walikua marafiki wa familia hata Wazazi sio tu Urais na amemsifu kikazi kwa umahiri wake ndio maana alifanya kazi naye kwenye wizra tatu za Afya, Mifugo na Ujenzi ambapo kwenye wizara zote alifanya vizuri.
Rais Mstaafu wa Awamu ya pili, Mhe. Ally Hassan Mwinyi amesema atamkumbuka Hayati JPM kwa fikra zake pevu zilizolenga kuitengeneza Tanzania Bora zaidi kiuchumi kupitia siasa ya uchapakazi na amepongeza moyo wa uzalendo uliozaa matunda ya Serikali kuhamia Dodoma ndani ya kipindi kifupi.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) bara Mzee Philip Mangula ametoa rai kwa watanzania na wanachama wa CCM nchini kutokata tamaa kwani yaliyopangwa kutekelezwa ndani ya kipindi fulani yameainishwa kwenye Ilani ya chama na amesema Hana wasiwasi na umahiri wa Rais Samia Suluhu.
Awali, akizungumza katika ibada ya maziko Askofu Gervas Nyaisonga Rais wa Baraza la Maaskofu Katoriki Tanzania (TEC) amewasihi waombolezaji kufanya maombolezo ya amani huku wakimkumbuka Hayati Rais Magufuli na ametoa rai kumtanguliza Mungu kwenye kipindi chote cha maisha.
Aidha, Askofu Nyaisonga amewasihi watanzania kufanya matendo yanayompendeza Mungu na kuacha kabisa tabia za Ushoga na Utoaji Mimba na akawataka wanasiasa kutokubali kupitisha sheria inayoruhusu matendo hayo maovu nchini.
Makamu mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoriki Tanzania, Askofu Flavian Kasala alitoa salamu za Baraza hilo na kusema watamkumbuka aliyekua Rais wa awamu ya tano wa Tanzania Hayati John Pombe Magufuli kwa kuweka nidhamu ya utendaji kazi hata taifa likapata maendeleo ya haraka ndani ya muda mfupi kupitia kauli yake ya Hapa kazi tu.
Aidha, Baraza hilo limemhakikishia Rais Samia Suluhu Hassan ushirikiano kwenye Utekelezaji wa majukumu yake ya kuiongoza nchi wakati wote kama walivyofanya hivyo kwa Marais waliopita akiwepo Hayati Rais John Pombe Magu fuli.
Kwa niaba ya Baraza kuu la Kiislamu Tanzania Mufti wa Tanzania, Shekhe Aboubakari Zuber alitoa salamu za rambirambi na akabainisha kuwa watamkumbuka Hayati Magufuli kwa upendo wa dhati kwa viongozi wa dini.
Msikiti wa Muhamad La Sirta unaojengwa Dar es Salaam na Rais Magufuli na akiusimamia mwenyewe maendeleo yake ulimfanya amkumbuke sana pamoja na msikiti wa Chamwino Dodoma alioujenga kwa michango yake mwenyewe na aliyoichangisha kutoka kwa wadau mbalimbali nchini.
" Sisi Kama watanzania tujenge ushirikiano na upendo, tuwe kitu kimoja nasi Kama watanzania tutakua bega kwa bega kukusaidia Mhe. Rais kwenye kila jambo utapotuhitaji," amesema Shekhe Zuber.
Mzee Samweli Bigambo, ametoa salamu za rambirambi kwa niaba ya wazee wa Chato ambapo amesema watamkumbuka Hayati John Pombe Magufuli kwa uchapakazi wake uliopelekea Miradi mingi ya maendeleo nchini na akamwomba Rais Samia Suluhu kumalizia miradi iliyoanzishwa na Hayati na amemuomba kuwa karibu sana na mjane mama Janeth Magufuli.
Amepongeza na kuishukuru serikali kwa sera ya wazee kwanza ambayo iliwapa kipaumbele kwenye kuhudumiwa kama hospitali na amemsihi kuhakikisha madawa yanakuwepo ya kutosha kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya.
Salamu kutoka vyombo vya ulinzi na usalama zimetolewa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Venancy Mabeyo ambaye alisema watamkumbuka Rais Magufuli kwa kujali vyombo vya ulinzi kwa kuharakisha huduma za kijeshi na utendaji uimarike.
Amesema, Hayati Dkt. Magufuli aliviimarisha vyombo vya Ulinzi huku akivishirikisha vyombo vya ulinzi na alivishirikisha kwenye shughuli za miradi ya maendeleo kama ujenzi wa uzio wa mirerani na ujenzi wa Ikulu ya Chamwino Dodoma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa