Rais Magufuli Afungua Tawi la Benki ya CRDB Chato Mkoani Geita
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefungua tawi jipya la Benki ya CRBD Wilaya ya Chato Mkoani Geita awapongeza kwa kuwa na zaidi ya matawi 250.
Akiwahutubia wananchi wa Chato Mheshimiwa Rais ameipongeza Benki ya CRDB kwa kutoa ajira ambapo wameajiri zaidi watumishi 3200 na kufikia mwaka kesho wataajiri watumishi wengine 800 hivyo kufanya idadi ya waajiriwa wa benki hiyo kufikia zaidi ya 4000.
Ameongeza kuwa serikali ya awamu ya tani inaunga mkono juhudi hizo kwa kuwa benki imejibu ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Aidha, amewataka wananchi wa Wilaya ya Chato na Mkoa wa Geita kuitumia benki ya CRDB kwa kuwa inaaminika na huduma zake ni nzuri na itaimarisha usalama wa fedha zao kwa maendeleo ya taifa.
Mheshimiwa Rais ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa kazi nzuri ya kuchukua hatua kwa benki ambazo maendeleo yake sio mazuri na ameitaka BOT kuchukua benki hizo kwa kuwa serikali haitatoa ruzuku,ameiomba CRDB kuchukua benki hizo na kupunguza riba ili wananchi waweze kukopa kwa maendeleo yao.
Akiwa Wilayani Chato Mheshimiwa Rais Magufuli amesema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kujenga meli kubwa mpya ambayo itafanya kazi ndani ya Ziwa Victoria kwa gharama ya shilingi bilioni 35.
Vile vile amewataka watanzania kuacha tabia ya kuandika mambo mabaya kuhusu serikali bali watangulize uzalendo kwa kutangaza mambo mazuri yanayofanywa na Serikali.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Ashatu Kijaji amesema kuwa Nchi ya Tanzania inaongoza kwa huduma za Kibenki Afrika na ni ya Sita duniani.
Kufunguliwa kwa Tawi la Benki ya CRDB Wilayani Chato kutatoa fursa ya wananchi kupata huduma za kibenki karibu na maeneo yao kwa kutunza fedha na kukopa mitaji kwa ajili ya maendeleo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa