RC GEITA AKUTANA NA UONGOZI WA SHIRIKA LA NDEGE TANZANIA WAKUBALIANA KUANZISHA WAKALA GEITA
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la ndege Tanzania (ATCL) Bw; Ladislaus Matindi na kukubaliana kufungua Wakala wa Shirika hilo Mkoani Geita.
Akizungumza Ofisini kwake baada ya mazungumzo hayo Mhandisi Robert Gabriel amesema Mkoa wa Geita upo kwenye maandalizi ya kufungua Ofisi za Wakala wa Shirika la ndege Tanzania ili kurahisisha na kuwa na usafiri wa anga wa uhakika kwa wananchi wa Geita na nje ya Geita.
Mhandisi Robert Gabriel ameongeza kuwa uwepo wa Shirika la ndege katika Mkoa wa Geita ni fursa kubwa ya kuutangaza Mkoa na rasilimali zake kwa kuwa kutakuwa na watu wengi wanaoingia ndani ya mkoa kutoka maeneo mbalimbali wakiwa na fedha hivyo biashara zitakua ikiwemo sekta ya Utalii kwasababu kutakuwa na usafiri wa Uhakika.''Mkoa wetu umekaa kimkakati kuna nchi za jirani za Rwanda na Burundi tutapata abiria kutoka huko ambao watakuja Geita wakafanya biashara na kufanya utalii,pia Mkoa unataka kuanzisha mnada mkubwa wa madini ya dhahabu hivyo uwepo wa huduma za ATCL utafungua mkoa huu kwa kiwango kikubwa''.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la ndege Tanzania Ladislaus Matendi amesema kuwa shirika hilo linawarahisishia wakazi wa Geita kutumia huduma za ATCL wasiwe na haja ya kwenda Mwanza kupata Tiketi bali wazipate hapa hapa Geita hivyo watazungumza na wafanyabiashara ili kuanzisha wakala. Amesema Mkoa wa Geita una fursa nyingi sana zikiwemo uchimbaji wa madini, bidhaa za Kilimo zinapatikana kwa wingi hivyo Geita inaangaliwa kipekee.Ameongeza kuwa Mkoa una vivutio vingi hivyo ni wakati wa ATCL kushirikiana na Mkoa, Bodi ya Utalii na TANAPA kunadi vivutio hivyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa