Mkuu wa mkoa wa geita mhandisi Robert Gabriel ameafanya ziara na kukagua miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa wilayani chato mkoani geita ikiwemo stendi ya mabasi makubwa na madogo pamoja na barabara zake, uwanja wa michezo, eneo la kijiji cha utalii na kumaliza ziara yake hiyo kwa kutembelea ujenzi wa kituo cha afya muganza leo aprili 9, 2019.
Katika ziara hiyo iliyowahusisha kamati ya usalama ya wilaya ya Chato, mhandisi Gabriel ameridhishwa na hatua ya ujenzi wa stendi hiyo inayojengwa katika kijiji cha Kahumo, Kata ya Muungano katika eneo la ukubwa wa ekari kumi na tano ikiwa ni awamu ya kwanza yenye asilimia 14 ya utekelezaji inayofanywa na mkandarasi mayanga contractors itakayogharimu bilioni 25 ambapo ipo hatua ya awali itakayogharimu bilioni 5.3 hatua inayomfanya mkandarasi kuiomba halmashauri ya wilaya ya chato kuhakikisha mtiririko wa fedha unakuwa mzuri ili mradi huo usisimame kwani ni mradi imara uliozingatia vigezo.
Pia Mhandisi Gabriel ametembelea ujenzi wa uwanja wa michezo wa chato unaojengwa kwa kwa hatua ya awali kwa fedha za wahisani Benki ya CRDB ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa halmashauri hiyo Eliud Mwaiteleke, hadi sasa fedha zilizotolewa milioni 50 pamoja na milioni 2.5 kutoka halmashauri zimewezesha uandaaji wa uwanja, usimikwaji wa magori, upandikizaji wa nyasi huku akitaja changamoto za kupungukiwa fedha na kutokuwa na uzio hali inayowapelekea kuchukua hatua mbalimbali za kutafuta fedha kwa wadau wengine ili kukamilisha jukwaa, eneo la kukimbilia, uzio pamoja na mifumo ya umwagiliaji, jambo linalomfanya mhandisi Gabriel kuomba kupewa bajeti ya uwekaji nyasi bandia ili kuona uwezekano wa kuharakisha ujenzi wa uwanja huo kwa manufaa ya uboreshaji wa michezo mkoani hapa.
Msafara wa mkuu wa mkoa ukaelekea kwenye eneo litakalowekwa kijiji cha utalii, lililopo katika kijiji cha Rubambangwe kata ya muungano lenye ukubwa wa ekari 30 karibu na mwambao wa ziwa viktoria ambapo kwa msisitizo, mhandisi Gabriel ameishauri halmashauri kuongeza eneo hilo angalau zipatikane ekari 40 nyingine kwani mambo yatayowekwa hapo yatahusisha utalii wa makabila yote 120 yanayopatikana nchini Tanzania, vilevile kuanzisha makumbusho ya viongozi ambapo wageni wataweza kufahamu historia ya nchi kwa namna ilivyopiganiwa na viongozi hadi kuendelezwa hivi leo.
Mhandisi Gabriel amesema, “tunazo tayari bilioni 10 za kuanzia, wataalam wanaendelea kuweka mipango sawa ili kuwezesha kuunganisha utalii wa ziwa viktoria, hifadhi ya rubondo, soko la dhahabu pamoja na uwanja wa ndege uliokaa kimkakati utakaotuletea watalii wa kutosha kupitia hifadhi zitakazotangazwa za Biharamulo, Burigi na Kimisi almaarufu (BBK), hivyo niwaalike wadau wa utalii njooni muwekeze kwa kujenga hotel za kisasa kwenye maeneo ya mwambao wa ziwa viktoria, hali ya hewa ni nzuri, maeneo ni mazuri”.
DC Chato Mhandisi Mtemi Msafiri amewakaribisha wadau wa uwekezaji akiwahakikishia kuwa kama ilivyo sera ya mkoa, Chato haina urasimu, hacheleweshwi mtu na mwitikio wa sekta binafsi ni mkubwa, hivyo wanaendelea kupima maeneo yaliyoko pembezoni mwa ziwa viktoria kwa kutambua kuwa, Chato ina mtandao mkubwa wa maji, hivyobasi ni vyema kuichangamkia fursa hiyo.
Mwisho, mhandisi Gabriel alimaliza ziara yake kwa kutembelea kituo cha afya Muganza kilichopo Kijiji cha Majengo kata ya Muganza ambapo hajafurahishwa na hatua za ujenzi wa kituo hicho pamoja na kwamba fedha zinakaribia kuisha lakini kazi bado iko nyuma hivyo kuagiza TAKUKURU kufanyia uchunguzi suala hilo ili kama kuna ubadhilifu aweze kuchukua hatua.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa