Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amefanya ziara ya kushtukiza katika kampuni ya Uchenjuaji Madini ya Dhahabu ijulikanayo kama Ombeo Group iliyopo Mtaa wa Nyamalembo Mjini Geita na kujionea namna ambavyo bado wapo wafanyabiashara wanaoendesha shughuli zao bila kufuata taratibu na hivyo kuendelea kutorosha utajiri wa Geita na kuikosesha serikali mapato yake halali kupitia rasilimali Madini ya Dhahabu.
Hayo yamejiri mapema leo tarehe 25.06.2018 majira ya asubuhi, ambapo Mhe. Mhandisi Gabriel aliambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Mkoa pamoja na waandishi wa habari ili kushuhudia tukio hilo.
Akiongea baada ya kupita na kuona shughuli zinazofanywa ndani ya eneo hilo ilihali shughuli hizo kuwa zimefungwa na Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Geita kwa zaidi ya siku thelathini nyuma, Mhe. Mhandisi Gabriel alisema, “ hapa kama mvayoona kazi zinaendelea na hii ni sehemu tu ndogo ya jinsi ambavyo mali zetu za Nchi zinachukuliwa; Serikali imekuwa ikipigana kulinda rasilimali zetu hizi adimu, Geita hii ni ya Dhahabu, Nchi hii inapambana kuhakikisha Sekta ya Madini inaleta matokeo makubwa katika uchumi wa Nchi, lakini kuna wizi mkubwa unafaywa na wageni kwa mgongo wa wenyeji”. Aliendelea kwa kutoa ONYO kali kwa wote ambao wanaendeleza jitihada za kutorosha Madini ndani ya Mkoa wa Geita na kwamba operesheni ndiyo kwanza imeanza hivyo waache mara moja .
Kwa upande wake Afisa Madini Mkazi Mkoani Geita Bw. Ali Said Ali alieleza kuwa, hapo awali Kampuni hiyo ilipigwa faini ya Shilingi Milioni Tatu na Laki Tano na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kutokana na uchafuzi wa mazingira iliyousababisha, pamoja na faini hiyo kutokulipwa hadi sasa, aliwafungia kufanya shughuli za uchenjuaji kwa kuwawekea Lakiri (Seal) mwezi mmoja nyuma mpaka hapo watakapokuwa wamekidhi matakwa ya kisheria ikiwemo kuwa na leseni hivyo naye kusikitishwa na kampuni hiyo kukutwa tena ikiendelea na uzalishaji. Hivyo alikazia kwa kusema, endapo kampuni itakutwa na makosa baada ya uchunguzi kukamilika, faini haitapungua Shilingi Milioni Hamsini na kutaifishwa kwa mali.
Mwisho, Mhe. Mhandisi Gabriel aliviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana na Ofisi ya Madini kufanya uchunguzi ,kujiridhisha kwa siku ya leo tu juu ya mambo yaliyokiukwa kwa mujibu wa sheria za nchi ili kuweza kuchukua hatua stahiki na kwamba hatamwonea yeyote bali sheria zitafuatwa.
Miongoni mwa waliokutwa ndani ya eneo la Kampuni hiyo ni raia wa kigeni Wachina wane, wanaume watatu na mwanamke mmoja, pamoja na Mtanzania mmoja mwanaume.
Geita ni mahala salama pa mwekezaji kuja kuwekeza akizingatia sheria na taratibu za nchi katika uendeshaji wa shughuli zake. Hivyo ni vyema kwa wafanyabiashara kuhakikisha wanafuata sheria na kulipa kodi stahiki kwa serikali wanapofanya shughuli zao ili kuepuka adhabu mbalimbali zitokanazo na uvunjaji wa sheria mbalimbali za nchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa