Katika kuboresha Sekta ya Afya hususan huduma ya damu salama, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita imekabidhi kwa uongozi wa hospitali ya rufaa, gari aina ya Mitsubishi Colt yenye namba za usajili STL 7159 kwaajili ya kusaidia huduma ya ukusanyaji damu salama kwaajili ya kuokoa maisha Agosti 8, 2019.
Akikabidhi gari hilo kwa Mganga Mfawidhi Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amesema lengo ni kuhakikisha wananchi wa mkoa wa geita wanaendelea kupata huduma za afya kwa kiwango stahiki huku akitoa wito wa utunzwaji na matumizi sahihi ya gari hilo kwa manufaa ya watanzania.
Amesema, “tunatoa gari hili kama kitendea kazi na hii ni kuhakikisha hospitali yetu ya rufaa ya mkoa inatoa huduma nzuri kwa wananchi mbalimbali wanaohitaji huduma za afya ili wasipoteze maisha kutokana na upungufu wa damu”
Utoaji wa gari hilo ni kufuatia ahadi ambayo mhandisi Gabriel aliitoa ya kuhakikisha anasaidia upatikanaji wa vitendea kazi katika sekta mbalimbali mkoani hapa, ikiwemo sekta ya afya.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa Bw.Deodatus Kayango amesema anaamini chombo hicho cha usafiri kitakuwa ni msaada kwa watumishi wa kitengo cha damu salama na utawala kwa ujumla na kitapunguza changamoto ya uhaba wa magari.
Akishukuru baada ya kukabidhiwa gari, Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Geita Dkt.Brian Mawala amesema, kama hospitali wanato shukrani za dhati kwa mhandisi Gabriel kwani kwao amekuwa baba, mlezi akihakikisha changamoto walizonazo zinashughulikiwa.
“asante mhe.mkuu wa mkoa kwa kutupa kipaumbele watoa huduma za afya hususan hospitali ya mkoa. Awali tulipata changamoto ya kutokuwa na usafiri wa hakika kukusanya damu salama, kuipeleka kwaajili ya vipimo katika maabara ya kanda kisha kurudisha na kuyasambaza majibu ya vipimo hivyo kwa wachangiaji, hatua hii ni ya kupongezwa. Na ninaamini sasa tutakuwa na damu salama kwa zaidi ya asilimia 90 kwakuwa tumewezeshwa kitendea kazi, lakini pia kama mzazi usituchoke kwani tuwapo na changamoto, tutaendelea kukufata", alimaliza Dkt.Mawala.
Naye Afisa Tawala Hospitali wa Rufaa Mkoa wa Geita Saashisha Mafuwe ameushukuru uongozi wa mkoa kupitia RC Gabriel akiahidi kuhakikisha gari hilo linatumiwa kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za utumiaji magari ya serikali na linatunzwa pia.
Amesema, “asante mhe.mkuu wa mkoa kwa kuendelea kuipenda sekta ya afya, kwakuwa kuipenda afya ni kuwapenda wananchi unaowaongoza, hivyo gari hili litachukua damu kwa wachangiaji, litaipeleka maabara ya kanda mwanza kwaajili ya vipimo, litarudisha vipimo, kisha kusambaza majibu kwa wachangia damu na endapo majibu ya damu yataonesha ugonjwa, basi mchangiaji ataitwa na kupatiwa tiba”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa