Jumla ya Shule za msingi tatu, vijiji vitatu na vituo vitatu vya kutolea huduma za afya kati ya washiriki 12 kutoka halmashauri za Nyang’hwale na Geita wameibuka kidedea kwa kujinyakulia fedha taslim pamoja na vyeti kutokana na shindano la usafi wa mazingira chini ya mradi wa majisafi na usafi wa mazingira na tendasia unaotekelezwa na shirika la WaterAID Tanzania, Amref Africa, wakishirikiana na Kampuni ya WEDECO Ltd
Akitoa pongezi kwa washindi hao agosti 1, 2019, mkuu wa mkoa wa geita mhandisi Robert Gabriel amelipongeza shirika la WaterAid Tanzania Kupitia mshirika wake WEDECO Ltd kwa kuanzisha shindano hilo ambalo binafsi anaamini ni chachu ya kuendelea kubuni mbinu bora na kuweka mikakati ili kupata ushindi kwa wale ambao hawakufanikiwa huku akisisitiza juu ya mabadiliko ya tabia kwenye matumizi sahihi ya choo bora na unawaji wa mikono kwa maji na sabuni ngazi ya kaya akisema nyumba ni choo isichukuliwe poa.
“ni matumaini yangu kuwa, matokea ya mashindano haya yatakuwa chachu ya taasisi zetu na vijiji vyetu kuwa na ari ya kuendeleza tabia ya usafi katika maeneo yote. Pia tuwapongeze WEDECO Ltd ambayo kipekee imetekeleza majukumu yake kwa kushirikisha ngazi zote kuanzia mkoa hadi vijiji, taasisi za serikali za elimu na afya pamoja na jamii katika vijiji vyote 12”, alisema mhandisi Gabriel.
Pia, mhandisi Gabriel alisema, huduma ya mafunzo, ufuatliaji shirikishi na mikutano imekuwa ni chichu ya mafanikio katika kutekeleza mradi huu huku akiwaomba washiriki kuyapokea matokeo ya shindano na kutoa mapendekezo, kuhamasisha na kuhimiza maendeleo ya usafi katika jamii zetu na kuwaunga mkono wadau kutengeneza jamii yenye mazingira safi na salama kwa vizazi vyote na kupunguza au kuondoa kabisa vifo visivyo vya lazima kwa akina mama na watoto ambavyo kwa kiasi kikubwa husababishwa na tabia za uchafu.
Mhandisi Gabriel amemaliza kwa kusema, “wajumbe wote kwa umoja wetu, hatuna budi kuwa mstari wa mbele katika kutokomeza tabia na matendo yote yanayodidimiza na kudhohofisha jitihada za mkoa katika kuinua hali ya upatikanaji wa maji safi na salama, usafi wa mazingira na tendasia, lakini pia niwakumbushe kuhusu kampeni ya Usichukulie poa Nyumba ni choo kupitia waratibu wote kuanzia ngazi ya mkoa, hadi mitaa na vitongoji vyote, kwamba ioneshe mwelekeo na uratibu wake uwe wa kimkakati na matokeo yaonekane kwani nitafanya ziara kuzunguka mkoa mzima kuhakikisha malengo tuliyowekeana yanafikiwa”.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa WEDECO Ltd Geita Mhandisi Baraka Mbalaga amesema, WEDECO LTD ikishirikiana na WaterAid pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Halmashauri za Wilaya za Nyang’hwale na Geita imekuwa inaendesha mradi wa uboreshaji wa afya ya mama na mtoto na kupunguza vifo vya wakina mama na watoto chini ya umri wa miaka mitano kwa kuhakikisha kuwa upatikanaji wa maji safi, usafi wa mazingira ni endelevu katika jamii.
Mradi huu umefadhiliwa na serikali ya watu wa Canada, chini ya mashirika makuu mawili, WaterAid Tanzania/ Amref Heath Tanzania, lengo kuu likiwa ni kuboresha afya ya mama na mtoto na kupunguza vifo vya mama na mtoto chini ya umri wa miaka mitano.
Mradi huu ni wa miaka mnne (2106 hadi 2020) unaotekelezwa katika Halmashauri za Wilaya mbili; Geita na Nyang’hwale katika ya kata 12 ambazo ni Kharumwa, Busolwa, Nyang’hwale, Kakora, Bukwimba, Nyugwa, Nyarugusu, Rwamgasa, Nyachiluluma, Nyakamwaga, Nkome na Nyamalimbe. Mradi umegusa taasisi za afya, elimu na jamiikatika kuhakikisha hali ya afya ya jamii kwa ujumla inaboreka na kuimarika.
Washindi wa shindano hilo ni kama ifuatavyo, Shule ya Msingi Chikobe Geita DC, Kijiji cha Bukwimba na Zahabati ya Busolwa Nyang’hwale DC waliibuka mshindi wa kwanza na kupata Tshs. 850,000 kila mmoja na washindi wa pili S/Msingi Zahanati na kijiji cha Chikobe Geita DC pamoja na zahanati ya busolwa kutoka Nyang’hwale walipata Tshs. 650,000 kila mmoja, na wa tatu S/Msingi Kakora , Kijiji cha Busolwa Kutoka Nyang’hwale na Kituo cha Afya Chikobe kutoka Geita DC wakapata Tshs. 500,000 kila mmoja pamoja na vyeti
Usafi ni Ustaarabu, Unaanza na Sisi
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa