Katika kuhakikisha Rasilimali za nchi hii zinatumika kama ilivyokusudiwa, vilevile huduma zinawafikia wananchi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Geita kwa Kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu Geita GGM, wameandaa Warsha ya Siku tatu kwa wadau na viongozi wa taasisi mbalimbali ndani ya mkoa yenye lengo la kutoa elimu juu ya mapambano dhidi ya Rushwa.
Akifungua Warsha hiyo iliyoanza tarehe 22.10.2018 katika ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Alphendo Mjini Geita, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel na Mgeni Rasmi amesema kuwa, semina hiyo ni muhimu kwa kuwa mla rushwa ni sawa na muuaji. Hivyo awashauri washiriki kujadili kwa kuweka wazi changamoto zinazopekelea mazingira ya rushwa kwa kuwa lengo ni kupona ugonjwa huo akisistiza uwepo wa ziara yake kusafisha watendaji wasiowajibika na walaji fedha za umma ndani ya Mkoa wa Geita.
Amesema, “wezi wajiandae, ziara ya mkoa yaja, kwa maana haiwezekani wilaya moja, majengo ya aina moja, mchoro mmoja halafu majengo yana gharama tofauti, hapa ni pa kujitafakari”. Akaongeza kusema kuwa”rushwa haitupi heshima, inachelewesha maendeleo, hivyo niwaombe viongozi wa dini muwe mabalozi wa kuelimisha haya, msiwe wa kuhubiri mafanikio tu, bali pia tukemee uovu kwenye mafundisho yetu”, hivyo kuwaambia wanahabari kufikisha ujumbe kwa watanzania kuwa Geita rushwa inachukiwa mno na kwa sasa ya uchunguzi utafanywa kimkakati na si kuwaachia TAKUKURU peke yao.
Mhandisi Gabriel ameeleza kuwa, angetamani dozi ama adhabu ya rushwa iwe kali zaidi kuliko ilivyo sasa ili watu watambue kuwa hakuna mchezo kwenye mapambano dhidi ya rushwa. Amewasihi watumishi wa umma kuwa na kazi mbadala za kujiingizia kipato kama vile kilimo, ufugaji n.k ili kuepuka vishawishi vya rushwa. Amesisitiza pia uwepo wa uwazi katika kamati za miradi ya jamii CSR, kamati za Wilaya na za Mgodi wa GGM na kujenga tabia ya uwazi.
Mkurugenzi wa Utafiti na Udhibiti kutoka Makao Makuu ya TAKUKURU Bi. Sabina Seja kwa upande wake amesema, hiyo ni hatua muhimu ya mapambano dhidi ya rushwa akisema kuwa msisitizo kwenye warsha hiyo ni kujadili kwa pamoja sababu mbalimbali za kuwepo rushwa miongoni mwa washiriki na kutafuta utatuzi wa changamoto hizo ili kudhibiti mianya yote, hivyo awasihi watumishi wa umma na Wanageita kwa ujumla kutojihusisha na vitendo vya rushwa ili kujiletea maendeleo, kisha kuwashukuru wadau GGM kwa ushirikiano.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Mgodi wa GGM Bw. Richard Jordinson amesema kuwa, GGM inayo furaha kufanya kazi na TAKUKURU katika uandaaji wa warsha hiyo, akisema warsha hiyo ni muhimu ili kusaidia kupunguza rushwa, si kwa Geita tu bali Tanzania kwa ujumla lakini pia angependa kuona miradi ya jamii kupitia CSR isihujumiwe au kuwa na vitendo vya rushwa.
Awali akisoma taarifa fupi mbele ya mgeni rasmi, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita Bw. Thobias Ndaro amesema warsha hiyo itamkumbusha mshiriki wajibu wa kupambana na kuzuia vitendo vya rushwa ili kuwaongezea wananchi imani ya serikali inayowaongoza na huduma na maendeleo kwa wananchi vitaonakana vikiwa halisi. Bw. Ndaro amesema pia anaamini kuwa, ushauri na mapendekezo ya washiriki yatapatikana ili kujua nini kifanyike katika kutokomeza rushwa Mkoani Geita.
Warsha hiyo imewakutanisha Maafisa wa Serikali, Watumishi wa Mgodi wa GGM, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Mashirika ya Umma na Binafsi, Taasisi za Fedha na Mifuko ya Jamii.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa